Home » » Majaliwa aagiza uongozi kituo cha afya ubadilishwe -ARUSHA

Majaliwa aagiza uongozi kituo cha afya ubadilishwe -ARUSHA

Written By CCMdijitali on Sunday, December 4, 2016 | December 04, 2016


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwafariji wakinamama waliolazwa kwenye wodi ya wazazi katika hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru wakati alipotembelea wodi hiyo na kukuta wakiwa wamelala watatu kwenye kitanda kimoja Desemba 4, 2016. 


⟺⟺⟺⟺⟺
 
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Frida Mokiti kubadilisha uongozi wa Kituo cha afya cha Levolosi baada ya kulalamikiwa na wananchi kuwa kinatoa huduma mbovu kwa wagonjwa, hususan wajawazito.

Pia amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kujenga hospitali za wilaya ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za rufaa.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana wakati alipotembelea Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, ambako alisema tatizo la msongamano wa wagonjwa hospitali za rufaa na hospitali nyingine ni lazima lipatiwe ufunguzi.

“Hatuhitaji kuwa na madaktari ambao wanasumbua wagonjwa. Daktari wa Mkoa hakikisha kile kinacholalamikiwa kule Levolosi kinatafutiwa ufumbuzi. Hapa Mount Meru hakikisheni mnaboresha mazingira ya vyoo kwenye wadi za wazazi pamoja na kujenga sehemu ya kuoshea vyombo kwa wagonjwa,” alieleza Waziri Mkuu.

Awali alipotembelea wodi ya akinamama wanaosubiri kujifungua, mmoja wa wagonjwa, Glory Paul anayeishi Olasiti jijini hapa alimweleza Waziri Mkuu kuwa mtoto wake alifia tumboni baada ya wauguzi na madaktari wa Kituo cha Afya cha Levolosi kuchelewa kumpatia matibabu.

“Wakati nahudhuria kliniki nishaambiwa na daktari kuwa natakiwa kujifungua kwa njia ya upasuaji na siwezi kujifungua kwa njia ya kawaida nilimwambia nesi kuwa natakiwa kufanyiwa upasuaji wakanikatalia na kunilazimisha nijifungue kwa njia ya kawaida ambapo ilishindikana na baada ya muda waliniambia kuwa mtoto amekufa na wananifanyia upasuaji ili kuokoa maisha yangu,” alieleza Glory.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia alisema amepokea maagizo ya Waziri Mkuu, Majaliwa, ambayo yanalenga kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kusisitiza kuwa awali alichukua hatua za kinidhamu kwa watoa huduma za afya kituoni hapo na ataendelea kusimamia nidhamu ya kazi ili kuondoa malalamiko kwa wananchi juu ya huduma za afya.

MWISHO

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waganga na Wauguzi wa hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru wakati al;ipoitembelea Desemba 4, 2016. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akielekea kwenye wodi ya wazazi katika hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru wakati a;lipoitembelea Desemba 4, 2016. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link