Imeandikwa na Veronica Mheta - Habari Leo
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli inasimamia nidhamu ya kazi na heshima kwa wananchi, hivyo kutaka kila mmoja atimize wajibu wake.
Aidha, imeonya kuwa fedha za miradi ya serikali ni za moto hivyo ziachwe sifanye shughuli zilizokusudiwa, kwani zikichezewa lazima zitaunguza mtu au watu.
Aliyasema hayo jana jioni alipozungumza na wananchi wa Jiji la Arusha waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Alisema serikali imeamua kupanua wigo wa kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na serikali yake kwa kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za serikali.
Alisema serikali inaendelea kuwahudumia wananchi na kuwataka wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia maendeleo ya wananchi huku akimpongeza Gambo kwa kufanya kazi za kuwahudumia wananchi.
Pia amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kukutana na watoa huduma wa magari ya Noah yanayosafirisha abiria maeneo mbalimbali ili kutatua changamoto zao ikiwemo usumbufu wa usafirishaji wanaopata.
Alimpongeza kwa kuwezesha kuibua ajira kwa vijana na kumwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia kuhakikisha vijana wanapewa maeneo ya kufanya biashara.
Waziri Mkuu pia alitoa rai kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuangalia jinsi ya kukusanya ushuru kwa kinamama wafanyabiashara wanaotembeza bidhaa zao kwenye mabeseni jijimo humo ili waweze kujikwamua.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alikabidhi pikipiki zaidi ya 200 kwa waendesha bodaboda ili waweze kujikwamua kiuchumi. Awali, kabla ya Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi, Gambo alimpongeza Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro (Chadema) kwa kuungana na falsafa ya Hapa Kazi Tu.
Alisema alipoingia mkoani hapo alikuta Diwani analipwa Sh 150,000 kila mwezi na vocha ya simu Sh 100,000.
“Tuliona hili hapana na tulikata fedha hizo za madiwani tukalipa madeni ya walimu. Kuhusu maeneo ya wazi, tumempa orodha Rais ya hayo maeneo na tunasubiri maamuzi yake kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema.
Picha ⇊⇊
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipoingia kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kuhutubia mkutano wa hadhara Jumamosi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Ndg Mrisho Gambo akiwatambulisha viongozi mbalimbali kwenye mkutano wa hadhara uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha. ⇅
Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha akiwasalimia wananchi waliohudhuria katika mkutano kwenye uwanja cha Sheikh Amri Abeid.
Mbunge wa viti maalum Bi Catherine Magige akiwasalimia wananchi waliohudhuria katika mkutano kwenye uwanja cha Sheikh Amri Abeid.
Waziri Mkuu akivishwa nguo za heshima ya jamii ya kabila la Kimasai katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja cha Sheikh Amri Abeid.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa akikata utepe ili kukabidhi pikipiki 200 zenye thamani ya sh.milioni 400 kwa vijana 200 wa Jiji la Arusha, ili kuweza kuwakwamua kiuchumi vijana hao ambao walikuwa wakiendesha pikipiki za watu ambazo hazina tija.
Pikipiki hizo zimechangwa na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Arusha baada ya Mkuu wa Mkoa huo Bw. Mrisho Gambo kubuni mpango huo ambao umewawezesha vijana kupata pikipiki bila riba wala dhamana.
Baada ya kukabidhi pikipiki hizo, Waziri Mkuu aliwataka vijana kuhakikisha wanakuwa waaminifu kwa kufanya kazi kwa bidii ili pikipiki ziweze kuwasaidia kuwainua kipato.
Mkuu wa Mkoa Mhe Gambo alisema pikipiki hizo zilizokabidhiwa kwa vijana hao zimetolewa sanjari na bima kubwa (Comprehensive Insurance) kwa vijana 200 ambapo kila Kata ilitoa vijana wanane .
Waziri Mkuu akikabidhi pikipiki jioni (Jumamosi, Desemba 3, 2016) mara baada ya kumaliza kuhutubia maelfu ya wananchi waliohudhutia katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja cha Sheikh Amri Abeid.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi kofia gumu ikiwa ni ishara ya kumkabidhi pikipiki katika tukio la kukabidhi pikipiki 200 kwa vijana wa bodboda wa Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abed jijini Arusha , Desemba 4, 2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipokuwa anaondoka kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha mara baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara Jumamosi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipokuwa anaondoka kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha mara baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara Jumamosi.
Picha zote na Katibu wa Siasa na Uenezi CCM Arusha - Jasper Kishumbua