Home » » Rwanda yatoa ya moyoni biashara nchini Tanzania

Rwanda yatoa ya moyoni biashara nchini Tanzania

Written By CCMdijitali on Friday, December 9, 2016 | December 09, 2016


Kwa ufupi
Alisema vikwazo vipo katika mamlaka za udhibiti na usalama wa bidhaa kwa kuwa licha ya kupitishwa na mamlaka za Rwanda, Tanzania huanza utaratibu upya.

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.Imeelezwa kuwa vikwazo visivyo vya kodi vinakwamisha biashara kati ya Tanzania na Rwanda.

Akizungumza juzi kwenye mkutano uliojadili mwelekeo wa biashara kati ya nchi hizo, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Francois Kanimba alisema licha ya juhudi za Serikali kuhakikisha zinafanya biashara pamoja, bado vipo vikwazo vinavyorudisha nyuma wafanyabiashara.

Alisema vikwazo vipo katika mamlaka za udhibiti na usalama wa bidhaa kwa kuwa licha ya kupitishwa na mamlaka za Rwanda, Tanzania huanza utaratibu upya.

“Utaratibu huu hupoteza muda na kuongeza gharama, iwapo tungeamini mamlaka za nchi zote mbili na bidhaa zikafikia sokoni, usumbufu wa aina hii usingekuwapo, ” alisema Kanimba.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema mkutano huo ulijadili suala hilo ili kupunguza vikwazo visivyo vya kikodi.

“Tunataka chakula kinachozalishwa nchini kikiingia Rwanda au kikija huku kama kimethibitishwa na mamlaka ya chakula na dawa ya nchi mojawapo, hakuna haja ya kwenda kuanza utaratibu huo upya, ” alisema Ngonyani.

Alisema yaliyojadiliwa yatawasilishwa kwenye mkutano ujao wa nchi za Afrika Mashariki na makubaliano ya nchi hizo kutekelezwa kwa pamoja.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dk Samuel Nyantahe alisema mkutano huo utaboresha maendeleo ya viwanda.


Dk Nyantahe alisema hali ya biashara kati ya nchi hizo ni asilimia 14, hivyo wataangalia namna ya kushirikiana zaidi.

“Unaweza kuona katika mkutano huu, Rwanda wamekuja na vifaa vya hospitali na dawa ambavyo mara kadhaa nchi imekuwa ikiagiza kutoka mataifa yaliyo mbali ilhali jirani vipo, hivyo inawezekana kuwasiliana na wahusika na kuwaunganisha na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na kununua kutoka hapa jirani badala ya kutumia gharama kubwa kuagiza kutoka mbali, ” alisema Dk Nyantahe.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link