Home » » Serikali yatenga bilioni 15/- kufunza vijana

Serikali yatenga bilioni 15/- kufunza vijana

Written By CCMdijitali on Saturday, December 10, 2016 | December 10, 2016

Kassim Majaliwa
 Mwandishi wetu - Jambo Leo
 
WAZIRI Mkuu Kassim Mjaliwa amesema Serikali imetenga Sh bilioni 15 za mafunzo kwa vijana zaidi 2,500 ili kuwajengea uwezo wa kuwa nguvukazi kwenye viwanda vinavyotarajiwa kujengwa nchini.

Alitoa kauli hiyo juzi kwenye sherehe za utoaji Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka 2016, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Tuzo hizo ziliandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).

Waziri Mkuu alisema Serikali imejielekeza kutoa mafunzo kwenye sekta za kipaumbele kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo kama kilimo biashara, mafuta, gesi, utalii, usafirishaji, ushonaji na bidhaa za ngozi.

Alisema jitihada zinaendelea kwenye maeneo mengine ili waajiri wawe na wigo mpana wa kupata wafanyakazi wenye stadi stahiki, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wao kuwa nguvukazi yenye ujuzi na umahiri mkubwa kwa lengo la kuongeza tija.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia tozo zinazotozwa na mamlaka tofauti za Serikali kwa huduma zinazofanana, kuwa wanazitambua na tayari mchakato wa kuainisha sheria zote zinazoonekana kukwamisha uwekezaji pamoja na mazingira ya biashara nchini.

“Lengo letu ni kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini ili yaweze kuvutia zaidi na mchakato huu unashughulikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

“Tunaomba mvumilie na mshirikiane nasi kuendelea kuainisha sheria zinazokwaza biashara, ili tuweze kuzijumuisha kwenye mapitio hayo,” alisema.


Hata hivyo, Waziri Mkuu alishauri waajiri nchini waendelee kufanya kazi  kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima mahala pa kazi.

Pia aliwasihi wafanyakazi kuongeza bidii na uaminifu ili waajiri waweze kupata faida, na kuwaboreshea maslahi yao.

Alisema: “Tunaposema Hapa Kazi Tu”, tunamaanisha kazi kwenye sekta zote za uzalishaji na utoaji huduma bora nchini, iwe sekta ya binafsi au utumishi wa umma.

“Nawasihi ndugu zangu Watanzania, wekeni nadhiri kwamba mwaka 2017 mtafanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuongeza tija na ufanisi mahala pa kazi.”


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista  Mhagama aliomba waajiri wawasaidie kuweka msukumo kwenye juhudi za kutoa mafunzo kwa ajili ya uzoefu na kuongeza ujuzi kwa kutoa nafasi kwa wahitimu kupata uzoefu kwenye maeneo yao ya kazi.

Hata hivyo, Jenista alisema anatambua umuhimu wa waajiri na wafanyakazi  katika utekelezaji wa sera ya maendeleo ya nchi hasa kwa kuongeza ajira kupitia sekta ya viwanda kwa asilimia 40 mwaka 2020, mafanikio ya mpango huo yanategemea mchango wa waajiri wa sekta binafsi.

Pia aliwapongeza ATE kwa kutambua umuhimu wa kuwekeza kwenye rasilimaliwatu hasa kwa kutoa tuzo katika eneo la kuendeleza vipaji, ambapo aliomba tuzo zijazo waongeze kigezo cha kupata mwajiri aliyetumia rasilimali zake kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi wake, ambao ndio chanzo cha kuinua tija na ushindani kibiashara.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk Aggrey Mlimuka alisema lengo la uaandaji Tuzo ni kutambua wanachama wenye sera nzuri za usimamizi wa rasilimaliwatu katika taasisi na kampuni mbalimbali wanachama nchini.

Alisema kuwa Tuzo hizo zinafuata mbinu za kisayansi na kitaalamu ili kuangalia umuhimu wa rasilimaliwatu katika kampuni za kibiashara kubwa na ndogo na za kati ili kuinua ujuzi wa wafanyakazi.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link