Home » » Ujasiriamali kufundishwa shuleni Zanzibar

Ujasiriamali kufundishwa shuleni Zanzibar

Written By CCMdijitali on Wednesday, December 7, 2016 | December 07, 2016


Imeandikwa na Khatib Suleiman - Habari Leo

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema inaangalia uwezekano wa somo la ujasiriamali kuliingiza katika mitaala ya elimu ya shule za msingi na sekondari Unguja na Pemba ili kuwawezesha wanafunzi kuwa na uelewa mzuri wa masuala hayo.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali ameyasema hayo wakati akifunga kongamano la wajasiriamali wa Unguja na Pemba katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani.

Balozi Amina amesema wakati umefika sasa kwa wanafunzi wakati wanapomaliza masomo yao kuwa na elimu ya ujasiriamali ambayo itawajenga kimaisha na kufanya vizuri masuala ya kibiashara kwa kuacha kutegemea ajira serikalini.

“Upo umuhimu mkubwa wa kuingiza masuala ya elimu ya ujasiriamali katika mitaala ya elimu kwa wanafunzi wa Sekondari kwa kuwawezesha kujitegemea wakati wanapomaliza shule na kuacha kutegemea ajira serikalini”.

Alisema ajira serikalini ni moja ya tatizo kubwa na njia pekee ya kulipatia ufumbuzi wake ni kuimarisha sekta binafsi.

Baadhi ya wajasiriamali waliozungumza baada ya kongamano hilo, walisema wanahitaji elimu zaidi itakayowawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuwapatia soko la haraka.

Mjasiriamali Asha Iddi anayetengeneza bidhaa za matunda ya kusindika, alisema upatikanaji wa soko na ubora wa bidhaa ni moja ya changamoto kubwa ambayo inahitaji kupatiwa ufumbuzi.

“Tumeanza kuzalisha bidhaa, lakini tunakabiliwa na tatizo la soko na wakati mwingine utaalamu wa kuzalisha bidhaa bora zaidi,” alieleza.

Kongamano la wajasiriamali mbalimbali Unguja na Pemba ambalo lilikuwa na mikakati ya kujenga uwezo kwa wajasiriamali lilifunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link