Mwandishi DEBORA CHARLES
Si kweli kwamba Serikali inakurupuka katika kufanya mambo yake, kila kinachofanywa na Serikali hii kimepangwa, kimeandikwa na kipo katika maandishi, WANANCHI tunapaswa kupuuza uzushi huu. Hii ni kauli aliyoitoa Katibu wa (NEC) Itikadi na Uenezi CCM Taifa Ndg. Humphrey Pole Pole alipokuwa akifanya mahojiano na muendesha mada katika kipindi cha "Mada Moto" Chanel Ten kuanzia saa 4:00 usiku 02/01/2016.
Akiendelea kutoa ufafanuzi juu ya mtazamo mbovu unaojengeka kwa baadhi ya watu dhidi ya Serikali Ndg. Humphrey Polepole alisema, tunayo DIRA ya maendeleo ya Taifa 2025 inayoainisha kuwa tunataka kujenga uchumi utakaotupeleka kwenye UCHUMI madhubuti na imara wa KATI unaolenga kuondoa umaskini kwa jamii wenye tabia/sifa mojawapo ya uchumi wa VIWANDA utakaoongeza ajira na uzalishaji mkubwa wa bidhaa zitakazotumika ndani na zingine kupeleka nje.
Dira hii inao Mpango wa kati (Long Term Perspective Plan) 2010-2025 ambao kwa namna ya pekee umeeleza nyanja mbalimbali katika kufikia uchumi wa viwanda. Mfano kabla ya kuwa na viwanda imebainishwa kuwa mazingira ambayo lazima yatengenezwe ni pamoja na;
1. UMEME WA UHAKIKA.
Jambo ambalo tayari Serikali kupitia maelekezo ya CHAMA CHA MAPINDUZI, imefauru kwa kiasi kikubwa mpaka sasa kulitekeleza, Serikali ilileta wawekezaji wakaweka gesi mpaka Ubungo, viwanda vingi vya uzalishaji kama vile kiwanda cha Simenti na Vinywaji viliaanza kutumia gesi hiyo. Kuna bomba kubwa kutoka Mtwara hadi Kinyerezi 1, 2,3 ambapo zaidi ya MegaWat 3000 zinazalishwa pia kuna mabwawa ya maji yanayoleta ongezeko kubwa la UMEME na kuufanya uwe wa kutosha na wa ziada. Uchumi wa viwanda unahitaji umeme wa uhakika kwa matumizi na uzalishaji.
2. NJIA ZA USAFIRISHAJI.
Tunaona serikali kupitia Maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi inavyotilia mkazo suala la Ujenzi wa RELI ya kati (Standard Gauge) ambapo pesa imeshakusanywa ili zoezi lianze haraka. Badala ya kutumia usafiri wa maroli ambayo kwa kawaida USAFIRISHAJI wake unagharimu pesa nyingi, sasa kutakuwa na uwezekano wa kusafirisha mzigo mkubwa zaidi kwa wakati mmoja na kwa gharama ndogo. Upanuzi wa bandari ili mizigo yetu kama vile Korosho na Simenti inayozunguka kutoka Mtwara Tanga mpaka Dar ije kwa bei nafuu kwa usafiri wa MELI kupitia bahari na baadae kusafirishwa kwenda Kigoma, Isaka n.k kupitia Reli ya TAZARA. Usafiri wa ANGA, Serikali imenunua Ndege nyingi Ili watu wakimbie haraka kwa shughuli za ndani za haraka.
KUHUSU SUALA LA MUENDELEZO WACHAKATO WA KATIBA MPYA.
POLEPOLE alisema, Dhamira kubwa ya Mageuzi ya Chama Cha Mapinduzi, ni kukirudisha Chama kwenye MISINGI ambayo kwayo Kilianzishwa na imeainishwa kwenye KATIBA.
Ikumbukwe kuwa Chama Cha Mapinduzi kimeamua kufanya MAGEUZI makubwa ambayo yanarudisha CHAMA cha Mapinduzi kwa Wanachama, Mageuzi haya yanakifanya Chama kujihusisha na shida za Wanachama, yanatengeneza mfumo wa Chama, Aina ya viongozi na mfumo mzima wa Uongozi na Utawala ambao unasikiliza watu, wananchi pamoja na wanachama katika yale yote ambayo wanataka kuyaona yamefanyiwa kazi na Serikali.
Chama Cha Mapinduzi kimeishauri Serikali kuanza kuwapatia watanzania UTAMU wa lile jambo linalokuja mbele kabla halijafika. Hivyo kipaumbele pekee ambacho Serikali kupitia maelekezo ya CCM kimeamua kuanza nayo ni kushughulika na kutendeakazi maoni yaliyotolewa na wananchi katika mchakato wa KATIBA MPYA.
Wananchi waligusia suala la MIIKO na MAADILI ya viongozi. Katika kulitendea kazi suala hili, Kiongozi wa Umma akishateuliwa, mbali na kiapo anachotoa mbele ya Rais, Kiongozi huyu anaapa tena ahadi ya uadilifu ya Kiongozi wa Umma (Kuapa tena kuenenda katika misingi fulani fulani mfano uwajibikaji, uaminifu, kusikiliza watu, unyenyekevu n.k.) mbele ya Mkiti wa Tume ya Sekretarieti ya Maadili ya Uongozi wa Umma. Hii inafanyika kwa sababu;
1. Serikali inaanza kujenga uzoefu kwa wananchi (wanaopewa dhamana ya uongozi) wafahamu kuwa uongozi ni dhamana.
2. Serikali kupitia maelekezo kutoka Chama Cha Mapinduzi inajaribu kuonyesha kuwa lazima iwe KALI kwa vitendo vyovyote vya ubadhilifu, rushwa, ufisadi na kukosa simile juu ya watu wanaojihusisha na mambo kama haya.
3. Bado Serikali ikaona iweke sheria zake vizuri ili watu wanaojihusisha moja kwa moja na makosa makubwa ya uhujumu uchumi (ufisadi) washughulikiwe kwa utaratibu maalumu wa kimahakama ili kuhakikisha kwamba mahakama za kawaida zinaendelea na mashauri ya kawaida lakini ambayo kwa hakika yanatetelesha uchumi wetu, yapewe kipaumbele kuhakikisha kwamba haki za watanzania zinapatikana.
Wananchi walisema wabunge wakae kwenye maeneo yao, Serikali kupitia maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi imeagiza kila mbunge akae kwenye jimbo lake, akae na kufanya siasa kwenye jimbo lake na ahamasishe wananchi kufanya siasa za maendeleo.
Wananchi walisema haiwezekani elimu bure ikawa mwisho darasa la saba, Serikali kupitia maelekezo ya CCM, pamoja na ugumu na changamoto likes inazokumbana nazo za kuanza Serikali mpya kabisa ikiwa ndiyo imetimiza mwaka mmoja tangu imeingia madarakani, imeadhimia kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Wakati mwingine mchakato wa Katiba ni mgumu hivyo ni vyema kujipanga na kuwa na uelewa wa pamoja.
Wakati mwingine ni vizuri mkaanza kufanya majaribio ya mambo haya na kuona yanakwenda namna gani.
Rais kwa mamlaka aliyopewa na katiba 1977, anayomamlaka ya kurekebisha vipande vyote na kuweka ambayo wanachi wanayataka na ndicho anachokifanya sasa. Mpaka tutakavyokuwa tumekaa kwenye usawa, wakati ambao vyama vya siasa vitafanya siasa za kistaarabu, siasa za kuheshimiana. Ni katika kipindi hicho, ikifika suala la katiba tunaweza kuzungumza lugha moja.
Angalizo, ukiona vyama vya siasa vinadai katiba kuliko wananchi, hapo tunageuza katiba kuwa jambo la kisiasa. Katiba ni jambo la wananchi, ndio maana Serikali imeamua kudumbukiza kwenye suala la utendaji mambo yote yaliyosemwa kwenye maoni ya Wananchi.