Home » » Ukatili wa kijinsia sasa basi Tanzania

Ukatili wa kijinsia sasa basi Tanzania

Written By CCMdijitali on Tuesday, January 3, 2017 | January 03, 2017

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliyemwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto 2017/18-2021/22 jijini Dar es Salaam. (Picha na Mroki Mroki).

 Imeandikwa na Katuma Masamba     - Habari Leo

UKATILI na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika jamii yetu ni miongoni mwa mambo ambayo yanayochangia taifa kutopata maendeleo.

Katika maeneo mengi hapa nchini vitendo hivyo vimeendelea kufanyika licha ya serikali kuwa na mipango mbalimbali ya kuzuia vitendo ambavyo pia ni kinyume na haki za binadamu. Matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto ni mengi licha ya kwamba mengine hayaripotiwi. Mfano katika wilaya ya Ilala pekee kuna kesi 1,094 dhidi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia zilizoripotiwa polisi kuanzia Januari hadi Septemba mwaka 2016.

Katika kutambua uzito wa suala hilo, mawaziri wa wizara 11 kwa mara ya kwanza wamekutana kwa ajili ya kuja na mikakati ya pamoja ya kutokomeza vitendo hivyo ambavyo vinaonekana kuongezeka kila kukicha. Mawaziri hao wamezindua Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ambao utatekelezwa kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2017 hadi 2022.

Utekelezaji wa mpango huo umelenga kushirikisha wadau katika jitihada jumuishi za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kusaidia waathirika wa ukatili na kupata huduma stahiki wanapofanyiwa nchini. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia. Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema jamii ina jukumu kubwa la kuhakikisha ukatili wa wanawake na watoto unapigwa vita kwa vitendo. “Serikali inaikumbusha jamii kupambana na vitendo vya ukatili kwani ukatili unafanyika kuanzia ngazi ya familia.

Ni jukumu la wananchi kutoa taarifa za ukatili ili vyombo vya dola vichukue hatua za kisheria.” Anasema matukio mengi ya ukatili yanasababishwa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na umasikini, mila na desturi potofu, malezi na makuzi mabovu na sheria kandamizi. Anasema wanazungumzia ubakaji na ulawati unaofanywa na watu wazima lakini cha kusikitisha zaidi kwa sasa kuna vitendo vya watoto wa kiume kulawitiana katika mazingira ya shule hivyo wizara hiyo imeamua kuanzisha madawati ya kuwalinda watoto kwenye shule za msingi na sekondari.

“Tunajua kama kuna mwalimu wa nidhamu lakini mara nyingi kwa mtoto mdogo mwalimu wa nidhamu anaogopwa, tunataka shule iwe sehemu rafiki kwa mtoto, kama amefanyiwa jambo ndani ya shule anakimbilia hapo ili kupata msaada wa haraka,” anasema. Anasema jambo lingine katika kutokomeza vitendo hivyo, wana mpango wa kuanzisha kamati za ulinzi na usalama wa mtoto katika mitaa na vijiji vyote nchini.

Ummy anaeleza kuwa wanawake pekee hawatafanikiwa hivyo wana mpango wa kuanzisha mtandao wa wanaume katika kila kata ambao watakuwa wakilinda na kutetea vitendo vya ukatili. Anaongeza kuwa Tanzania yenye maendeleo, usawa wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni itaweza kufikiwa ikiwa kila mmoja atashiriki katika kuwalinda watoto na wanawake.

Akielezea mpango huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga anasema kabla ya kuandaliwa kwa mpango kazi huo, Tanzania ilikuwa na mipango kazi nane ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Anasema kuwa mipango hiyo haikuwa na mfumo wa pamoja wa ufuatiliaji na tathimini. Vile vile kutokana na madhara ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maendeleo ya nchi Umoja wa Mataifa, na wakuu wa nchi wanachama waliazimia kwa pamoja kutokomeza ukatili huo kupitia utekelezaji wa lengo namba tano na sita ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030.

“Tanzania ni kati ya nchi nne za kwanza duniani na nchi pekee katika Bara la Afrika iliyowezeshwa kupitia jukumu lililoanzishwa la kusaidia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuandaa mpango wa kuzuia na kudhibiti ukatili,” anasema. Akielezea mpango huo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Afya, Emmanuel Achayo anasema mpango kazi huo una maeneo makuu manane yatakayotekelezwa na wadau wa maendeleo ya wanawake na watoto.

“Maeneo hayo ni kuimarisha uchumi wa kaya, uzuiaji wa mila na desturi zenye madhara na uboreshaji wa mazingira salama katika jamii,” anasema. Kwa mujibu wa Achayo maeneo mengine ni kuendeleza mazingira salama ya mafunzo shuleni na stadi za maisha na kuhuisha mahusiano, malezi na makuzi katika familia, utekelezaji na usimamizi wa sheria, utoaji huduma kwa waathirika na uratibu. Mengine ni ufuatiliaji wa tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa miaka mitano kuanzia mwaka 2017/18 hadi 2021/22.

Mpango huo unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa baada ya miaka mitano ya utekelezaji kwani utawezesha kuondoa ukatili kwa asilimia 50 kwa wanawake na pia na watoto ifikapo mwaka 2021/22 na hivyo kuleta mabadiliko makubwa kwa kuwa na familia salama na jamii yenye utulivu. Mpango umeweka mfumo fungamanishi wa utaratibu, ufuatiliaji na tathmini ambao utaratibiwa katika ngazi ya Taifa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ngazi ya mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa na ngazi ya Halmashauri na Wakurugenzi Watendaji.

Wakizungumzia utekelezaji wa mpango huo mawaziri hao wanasema watasimamia kwa nguvu zao zote kuhakikisha kuwa mpango kazi huo unafanikiwa, ili kufikia malengo ya kutomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango anasema, vitendo vya ukatili kwa sasa Watanzania wanatakiwa kusema basi kwani hata wanyama ambao wanaongozwa kwa silika hawawezi kufanya vitendo hivyo.

Anaendelea kusema athari na madhara ya kuendelea kwa ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni kubwa kiuchumi. Ukatili dhidi ya wanawake na watoto huchochea kuongezeka kwa umasikini jambo ambalo ni kinyume cha dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na mipango mingine ya maendeleo na mipango ya Kimataifa kama Malengo Endelevu ya Milenia (SDG’s). Anaongeza kuwa maendeleo endelevu na Tanzania ya viwanda itakuwa ngumu kufikiwa kama nguvu kazi ya sasa ambayo ni Wanawake na nguvu kazi ya kesho ambayo ni watoto wanaendelea kuathiriwa na ukatili uliopindukia.

Anasema mpango kazi huo unatarajiwa kugharimu Sh bilioni 267.4 kwa kipindi cha miaka mitano ambapo uatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla. Dk Mpango pia ameziagiza Wizara, Idara na taasisi za serikali, mikoa, wilaya pamoja na mamlaka za mitaa kuhakikisha zinazingatia mpango kazi huo kwa kutenga fedha katika bajeti zao kuanzia mwaka wa fedha 2017/18 ili kukidhi utekelezaji wa mpango huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama anasema, mbali na watoto wengine ambao maumbile yao yamejitosheleza, kumekuwa na ukatili mkubwa kwa watoto wenye ulemavu. Alisema serikali itahakikisha mpango kazi huo unatekelezeka kwa uwazi huku ukitoa huduma bora inayotakiwa, pia kuhakikisha mpango huo unaenda na gharama halisi ili kufikia malengo kwa muda uliopangwa.

Ofisi hiyo pia itahakikisha mpango kazi huo unahusishwa na mipango ya serikali katika ngazi zote, huku ikisimamia rasilimali fedha zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza mpango huo zinatumika katika malengo husika na si kufanya kazi nyingine. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema, serikali inataka kupitia sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ili kubaini mapungufu ambayo wadau wameyaona na kuyafanyia marekebisho.

Alisema pia wanaangalia namna ya kupanua wigo wa fursa kwa wanawake na watoto katika kutafuta haki na hatua mojawapo ya kufanikisha suala hilo ni kuanzisha mfumo wa msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Alvaro Rodriguez alisema, dhamira ya serikali imechangia katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika chini ya mpango mpya wa Ushirikiano wa Kimataifa katika kukomesha ukatili dhidi ya watoto. Rodriguez alisema malengo ya dunia yanataka kumaliza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto na badala yake kuwekeza katika kuwawezesha na kuwalinda

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link