Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Taasisi ya Maendeleo ya Utalii Zanzibar, Mh. Rashid Ali Juma, kulia ya Balozi Seif ni Mkurugenzi wa Thomas Cook Group Bwana Michael Scheidler na Mjumbe wa Kampuni hiyo Bwana Bart Schooppe.
Bwana Amin Msools wa Hoteli ya Nepmne ya Zanzibar yenye uhusiano wa kibiashara Kampuni ya Thomas Cook Group akifafanua jambo wakati wakizungumza na Balozi Seif hayupo pichani.
Kushoto kwa Bwana Amin ni Kiongozi mwenzake wa Hoteli ya Nepmne Bwana Mohamed Bhaloo na wa kwanza kutoka kushoto ni Waziri wa Taasisi ya Maendeleo ya Utalii Zanzibar, Mh. Rashid Ali Juma.
Balozi Seif akimkabidhi mlango wa Zanzibar {Zanzibar Door} Meneja wa Kampuni ya Thomas Cook Group Bwana Michael Scheidler kama ishara ya kumkaribisha kuendelea kuwekeza vitega uchumi vyao Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif kati kati akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Makampuni ya Thomas Cook Group na Hoteli ya Nepmne mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Kulia ya Balozi Seif ni Meneja wa Kampuni ya Thomas Cook Group Bwana Michael Scheidler na Kiongozi wa Kampuni hiyo Bwana Bart Schooppe.
Kushoto ya Balozi Seif ni Kiongozi wa Hoteli na Nepmne Zanzibar Bwana Amin Msools, Waziri wa Taasisi ya Maendeleo ya Utalii Zanzibar, Mh. Rasid Ali Juma pamoja na Bwana Mohamed Bhaloo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya Utalii ya Thomas Cook Group yenye Makao Makuu yake Nchini Ujerumani Bwana Michael Scheidler amesema Zanzibar inapaswa kuwa makini katika kusimamia miradi inayoanzishwa ndani ya Sekta ya Utalii kwa lengo la kuhifadhi mazingira yaliyopo.
Alisema kasi kubwa ya watalii na wageni wa Kimataifa wanaoamua kuvitembelea Visiwa vya Zanzibar inatokana na mazingira mazuri ya Rasilmali zilizopo pamoja na maumbile ya asili yanayovipamba Visiwa hivi.
Bwana Michael Scheidler na Ujumbe wake alieleza hayo wakati alipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar baada ya kufanya ziara fupi ya kuangalia mazingira ya Zanzibar pamoja na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Sekta inayosimamia Utalii Zanzibar.
Alisema mazingira ya Zanzibar yanayojumisha fukwe, misitu, vyakula vya viungo pamoja na ukarimu wa watu wake lazima yalindwe kwa njia yoyote ile ili lile lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kuifanya Sekta ya Utalii kuwa muhimili wa Uchumi wa Taifa iweze kufanikiwa vyema.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya Utalii ya Thomas Cook Group ameelezea faraja yake kutokana na mashirikiano mazuri yaliyopo kati ya Serikali na Taasisi za Uwekezaji katika miradi iliyomo ndani ya sekta ya Utalii.
Bwana Michael aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zake za kuendelea kuimarisha miundo mbinu mbali mbali ya Kiuchumi ikiwemo ile ya Sekta ya utalii.
Hata hivyo Bwana Michael alisema katika kuona Sekta ya Utalii inazidi kushika kasi suala la Watalii kurahisishiwa upatikanaji wa viza na vibali vya kuingia Nchini linahitaji kushughulikiwa vyema.
Alisema utaratibu wa kulishughulikia suala hilo utasaidia kuondoa urasimu jambo ambalo litatoa fursa nzuri kwa Watalii walioamua ghafla kufanya matembezi Zanzibar baada ya kupata sifa na haiba yake kupitia mitandao na hata wageni waliowahi kutembelea kabla.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Mheshimiwa Rashid Ali Juma ambae alikuwepo kwenye mazungumzo hayo alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshaamua Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar { ZITO } kukiunganisha na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA }.
Waziri Rashid aliueleza Ujumbe huo wa Viongozi wa Kampuni ya Thomas Cook Group kwamba hatua hiyo imelenga kuzalisha Wataalamu wa Sekta ya Utalii ambao baadaye watasaidia kuimarisha eneo hilo kwa ajili ya Uchumi wa Taifa.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushauri Uongozi wa Kampuni ya Thomas Cook Group kufikiria kutoa mafunzo kwa watendaji wa Mahoteli ili kutoa huduma katika kiwango kinachokubalika Kimataifa.
Balozi Seif alisema Kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa katika shughuli za Kiutalii unaoweza kusaidia pia watendaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar ambao hutoa huduma kwa watalii wa Daraja kwanza Duniani baadhi yao hutembelea Visiwa vya Zanzibar.
Aliipongeza Kampuni ya Thomas Cook Group kwa kusaidia kuimarisha Sekta ya Utalii Visiwani Zanzibar kupitia Watalii wa Daraja la kwanza wanaofika Zanzibar kwa uratibu wa Kampuni hiyo.
Balozi Seif alieleza kwamba hatua ya Kapuni hiyo kwa kiasi kikubwa imeongeza mapato ya Taifa sambamba na kutoa ajira kwa vijana wazalendo wanaobahatika kutoa huduma kwa watalii hao wa daraja la kwanza.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliufahamisha Uongozi wa Kampuni hiyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko katika jitihada za kuendelea kuimarisha miundombinu katika azma yake ya kuona mafanikio ndani ya sekta hiyo yanaleta matumaini.
Alisema ujenzi wa eneo la maegesho ya ndege kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu ni miongoni mwa miundombinu hiyo.
Balozi Seif alieleza kwamba Sekta ya Utalii Zanzibar hivi sasa imepewa nafasi ya kwanza na Serikali Kuu katika uchumi wa Taifa katika ukusanyaji wa mapato na kutoa ajira pana zaidi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/2/2017.