Home » » Balozi Seif aongoza Kikao cha Wajumbe wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar

Balozi Seif aongoza Kikao cha Wajumbe wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar

Written By CCMdijitali on Wednesday, February 8, 2017 | February 08, 2017

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akikiongoza Kikao cha Siku moja cha Wajumbe wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar kilichokutana Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Kikao hicho cha Siku moja kilijadili Muhtasari wa Taarifa ya Tathmini ya Sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar  zilizofanyika Januari 12 mwaka huu wa 2017.


Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud, Waziri wa Habari Mh. Rashid Ali Juma, Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdani Makame na Balozi Silima Kombo.


Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh. Issa Haji Ussi, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idrissa Muslim Hijja, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman na Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Mwnajuma Majid.


Picha na – OMPR – ZNZ.



Press Release:-


Maadhimisho ya Sherehe  za kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar  ya mwaka 1964 yaliyofikia kilele chake Januari 12 mwaka huu wa 2017 katika uwanja wa amani mjini Zanzibar yamefanikiwa vyema na kufikia kiwango kilichokusudiwa.

Mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano mkubwa uliyoonyeshwa baina ya Viongozi wa Kitaifa na wale wa Taasisi za Serikali na binafsi, Viongozi wa Mikoa, Wilaya pamoja na Wananchi katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

Hayo yalibainika wakati wa Mkutano wa Siku moja wa Wajumbe wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa  Zanzibar  walipokutana chini ya Mwenyekiti wake  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kujadili tathmini za sherehe hizo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Akiwasilisha Muhtasari wa Taarifa ya maadhimisho hayo ya sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar  kwa Wajumbe hao Mkurugenzi wa Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar Bibi Riziki Daniel Yussuf  alisema ushiriki wa Wananchi kwenye miradi tofauti iliyowekwa mawe na msingi na kuzinduliwa imethibitisha mafanikio hayo.

Mkurugenzi Riziki alisema jumla ya matukio  60 yalizipamba sherehe hizo iliyojumuisha miradi 32 iliyofunguliwa rasmi, 19 kati ya hiyo iliwekewa mawe ya msingi ikiwemo ile ya Kijamii.

Alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sherehe hizo lakini zipo changamoto zilizojitokeza kama Taasisi  na Wizara za Serikali kuchelewesha  kuwasilisha  miradi yao kwa wakati uliopangwa jambo  ambalo limepelekea kuchelewa kuandaliwa kwa ratiba ya sherehe hizo.

Alisema kukatishwa kwa burdani za ngoma  zilizopangwa kufanyika baada ya Hotuba ya Mgeni rasmi kwenye Kilele cha  sherehe za maadhimisho hayo Uwanjani Amani kumetokana na kupindukia kwa kiasi kikubwa muda uliopangwa wa kumalizia sherehe hizo.

Akiahirisha  Kikao cha Wajumbe wa Halmashauri  ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa  Zanzibar Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi alisema kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Wananchi wakizingatia zaidi uzalendo ndiyo inayochangia kufanikisha kudumu kwa sherehe za Mapinduzi Zanzibar kila Mwaka.

Balozi Seif aliwahakikisha Wajumbe wa Halmashauri hiyo pamoja na Wananchi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itayazingatia Mapendekezo yote yanayotolewa katika kuona mapungufu yanayojitokeza wakati wa Maadhimisho ya Sherehe hizo yanachukuliwa hatua zinazostahiki.

Mapema wakichangia Muhtasari wa Taarifa ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar Wajumbe wa Mkutano huo wamependekeza Wizara ya Fedha na Mipango iweke utaratibu mbadala wa upatikanaji wa fedha za matumizi ya sherehe hizo.

Walisema upatikanaji wa fedha hizo mapema utaziwezesha shughuli zote zinazokusudiwa  kutekelezwa ndani ya sherehe hizo kuanza mapema kwa maandalizi ya sherehe hizo ili kusaidia kupatikana kwa ufanisi mzuri.

Wajumbe hao walisisitiza umuhimu wa wasimamizi wa matukio yote yanayopangwa kufanyika katika ratiba ya Uwanjani ni vyema wakazingatia wakati uliopangwa ili kunusuru shughuli nyengine kukatwa hali ambayo pia husababisha hasara na usumbufu.



Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
8/2/2017.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link