Mchango huo aliutoa Ikulu ndogo ya Mkoa wa Katavi akijiandaa kurejea Zanzibar baada ya kumaliza ziara yake ya siku tatu Mkoani humo iliyoambatana na uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Wazee waasisi wa Kamati ya siasa ya Mkoa wa Katavi wakibadilishana mawazo na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani hapo ofisi ya CCM Mkoa wa Katavi.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi Nd. Abdalla Mselem mara baada ya kukutana na Viongozi wa Kamati ya Siasa ya Mkoa huo.
Kulia ya Ndugu Mselem ni Waziri wa Kazi, Uwezeshaji,Wazee, Vijana Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Moudline Cyrus Castico.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Wanachama wa CCM kujipanga vyema katika kuhakikisha Viongozi wanaowachagua katika ngazi mbali mbali ndani ya Chama chao wanakuwa mahiri kwa ajili ya kueperusha bendera ya ushindi wa Chama hicho ifikapo mwaka 2020.
Alisema upembuzi wa wanachama hao katika kuwatafuta viongozi mahiri ndio njia pekee na sahihi itakayokiwezesha Chama cha Mapinduzi kuendelea kuongoza Dola ya Tanzania Bara na Zanzibar katika Miaka mingi ijayo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akibadilishana mawazo na Viongozi wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi ya Mkoa wa Katavi kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Chama hicho Mkoa mara baada ya kumalizika kwa sherehe za Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika Mkoani humo.
Aliwaeleza Viongozi hao kwamba Chama pekee chenye dhamana na imani ya kuliongoza Taifa la Tanzania bila ya kutetereka ni Chama cha Mapinduzi kutokana na Historia yake iliyotokana na vyama vya Ukombozi vya TANU na Afro Shirazy Party.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema CCM ndio Chama Pekee Nchini Tanzania kilichoainisha ndani ya Ilani na Sera zake kuahidi kutunza Amani na Utulivu wa Taifa Uliopo sehemu zote za Jamuhuri ya Mauungano.
Aliwahimia Wanachama wa Chama hicho pamoja na Wananchi wote Nchini kujitahidi kuitunza Amani ya Taifa na kujiepusha na vishawishi vya baadhi ya Watu wanaokusudia kutaka kuichafua kwa malengo yao binafsi.
“ Wana Chama cha Chama cha Mapinduzi pamoja na Wananchi wote wasikubali kuruhusu watu wachache wanaojaribu kutaka kuichezea amani ya Nchi”. Alisema Balozi Seif Ali Iddi.
Alisema wapo baadhi ya Raia wa Mataifa Jirani waliyoamua kuzihama Nchi zao na kuomba kupatiwa Uraia wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kukimbia vita visivyokwisha vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokana na sababu za kuichezea amani ya Nchi hizo.
Balozi Seif alisema Watanzania wanapaswa kulazimika kuwa makini na mitego kama hiyo inayoashiria kuchezewa kwa amani hiyo na vyenginevyo ile sifa inayoelezwa kila mara na jumuia za Kimataifa ya kuwa Tanzania ni Kisiwa cha Amani inaweza kuyayuka.
Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi Ndugu Abdalla Mselem alisema Wana CCM na Wananchi wa Mkoa wa Katavi wameomba fursa zozote zinazotokezea za Kiserikali na Kichama zifikiriwe kupelekwa Mkoani humo kwa vile bado ni mpya.
Nd. Mselem alisema Mkoa wa Katavi ulioasisiwa Mwaka 2012 ulitokana na Sensa ya Idadi ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 iliyopelekea mabadiliko ya mgao wa Mikoa kufuatia ongezeko la Idadi ya Watu katika maeneo mengi nchini.
Wakati huo huo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif alikutana kwa mazungumzo mafupi na Kamati ya Waasisi wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Katavi kwenye jengo la Ofisi ya CCM ya Mkoa huo.
Katika mazungumzo hayo Waasisi hao walimlalamikia Balozi Seif juu ya tabia mbovu ya baadhi ya Watendaji Wakuu wa Serikali wanapofanya ziara Mikoani wanakwepa kukutana na Viongozi wa Chama Tawala.
Waasisi hao walisema kitendo cha Watendaji hao kinaashiria dharau zisizo na msingi wakisahau kwamba uwajibikaji wanaoutekeleza unatokana na Sera za Chama cha Mapinduzi zilizopata ridhaa ya Wananchi walio wengi na hatimae kuunda Serikali iliyowaweka Madarakani.
Balozi Seif Ali Iddi alikuwa Mkoani Katavi kuzindua rasmi Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein zitakazochukuwa siku 195 ndani ya Mikoa yote 31Tanzania Bara na Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/4/2017.