Rais John Magufuli akijaribu kuendesha trekta katika kiwanda cha kutengeneza matrekta aina ya Ursus kilichopo Kibaha mkoani Pwani jana baada ya kuzindua mradi wa kutengeneza matrekta hayo. (Picha na Ikulu).
RAIS John Magufuli amezindua viwanda vikubwa vitatu na mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa mabomba makuu kutoka Mlandizi hadi Dar es Salaam, katika siku ya pili ya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani jana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, kwanza, Rais Magufuli alizindua kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Tanzania Ltd kilichopo katika eneo la viwanda Kibaha ambacho kina uwezo wa kutengeneza mifuko ya sandarusi 53,000 kwa siku kwa ajili ya kuhifadhia mazao.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Mtanzania, Joseph Wasonga kimeajiri watu 110 na kimejengwa kwa gharama ya takribani Sh bilioni nane. Aidha, Dk Magufuli alizindua mradi wa kutengeneza matrekta 2,400 aina ya Ursus ambao utagharimu Sh bilioni 55, na matrekta hayo yatasambazwa nchi nzima kwa ajili ya kuboresha sekta ya kilimo.
Mradi huo unamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na utazalisha matrekta ya aina 6 zenye nguvu ya kuanzia HP50 hadi HP 85. Pia jana, Rais Magufuli alizindua kiwanda cha chuma cha Kiluwa Steel Group kilichopo Mlandizi ambacho katika awamu hii ya kwanza kina uwezo wa kuzalisha tani 500,000 za nondo kwa mwaka na awamu ya pili kitaongeza uzalishaji hadi kufikia tani milioni 1.2 kwa mwaka.
Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema kiwanda hicho kinachomilikiwa na Mtanzania Mohamed Kiluwa kwa asilimia 51, asilimia 49 zinamilikiwa na mwekezaji kutoka China ikiwa ni mwendelezo wa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya China na Tanzania.
Aidha, Shirika la Reli Tanzania (TRL) limejenga njia ya reli ya kilometa 3.5 inayounganisha kiwanda hicho na reli ya kati ikiwa ni juhudi za kurahisisha usafirishaji wa malighafi na vyuma vinavyozalishwa kiwandani hapo kwenda ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika miradi hiyo, Rais Magufuli alipongeza uwekezaji huo na akaagiza vyombo vinavyohusika kutoa vibali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hapa nchini viondoe urasimu ambao umekuwa ukiwakatisha tamaa wawekezaji kujenga viwanda.
Dk Magufuli alitoa mwito kwa wamiliki wa viwanda hivyo kujali maslahi na usalama wa wafanyakazi waliowaajiri, amezitaka benki nchini kujielekeza kufanya biashara na wananchi kwa kuwakopesha mitaji wafanyabiashara na wajasiriamali badala ya kutaka kufanya biashara na serikali na ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha viwanda vya chuma vinatumia malighafi za hapa nchini kutoka Mchuchuma na Liganga.
Leo Rais Magufuli atakamilisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani kwa kuzindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona Drink Ltd, kuzindua kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agric Company na kuzindua mradi wa barabara ya Bagamoyo – Msata.