Home » » Magufuli ‘amtumbua’ Mutalemwa Dawasa

Magufuli ‘amtumbua’ Mutalemwa Dawasa

Written By CCMdijitali on Thursday, June 22, 2017 | June 22, 2017


     Imeandikwa na Shadrack Sagati

RAIS John Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam, (Dawasa), Archad Mutalemwa ‘kuachia ngazi’ kwa maelezo kuwa amekaa muda mrefu katika mamlaka hiyo.

Rais pia amemwagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji kuhakikisha anamaliza mkanganyiko uliopo kati ya Dawasa na Kampuni ya Maji Safi Dar es Salaam (Dawasco) juu ya uendeshaji wa huduma ya maji na pia amemwagiza namna ya kuangalia kuunda bodi moja ya maji; badala ya kuwa na bodi mbili zinazosimamia taasisi hizo mbili.

Mbali na hilo, alisema taasisi za serikali zisizolipia huduma ya maji zinapaswa kukatiwa huduma hiyo na kwamba wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa wilaya ambao taasisi zao nyeti zitakatiwa maji, wajihesabu kuwa wameshindwa kazi kwa sababu fedha zinatolewa kulipia huduma hiyo muhimu.

Rais Magufuli pia ameiagiza Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhakikisha kwamba wafanye kila linalowezekana mji wa Kisarawe mkoani Pwani upatiwe maji haraka na pia wakamilishe mradi wa maji wa Lindi ambao alisema umekaa kwa muda mrefu bila kukamilika.

Dhambi za wizara
Akizindua mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa mabomba makuu kutoka Mlandizi kwenda Kibamba, Dar es Salaam, Rais Magufuli alitaja upungufu ya wizara ni kuwepo kiwanda jijini Dar es Salaam ambacho kilifunga bomba la maji bila kupitishiwa kwenye mita.

Alisema kinatumia maji mengi, lakini hawalipi bili. Pia alisema kuna kampuni moja inajenga barabara ilikuwa inatumia maji ya Dawasco bila kulipa ankara zao. “Sasa kama hao matajiri hamuwadai ankara zenu, inakuwaje wananchi hawa maskini mnakuwa na viherehere vya kwenda kuwadai bili zao,” alieleza Rais Magufuli katika hotuba yake kwa wananchi.

Pia alisema kuna wafanyakazi wa Dawasco ambao anawafahamu wanaouza maji na fedha zinaenda kwenye akaunti zao na akasisitiza kuwa anafahamu hadi akaunti zao. Alimwagiza waziri alifanyie kazi yeye mwenyewe.

“Rekebisheni dhambi zenu zilizopo, hapa Ruvu mmepata A, lakini kule kwingine mmepata C maana mambo yenu hayaendi vizuri,” alisema Rais. Amvaa bosi wa Dawasa Rais Magufuli katika hotuba yake alihoji, “Kuna wanaouliza hivi Mutalemwa utastaafu lini?

Maana nimeanza kukusikia nikiwa bado sekondari. Mzee wangu jiandae kustaafu, unaweza kuwa na mwili mzuri; lakini umri umekwenda tunataka kukutumia kwa kazi zingine za taifa hili. “Hivyo nakuomba mzee wangu jiandae kustaafu kwa haraka kabla ya mabaya hayajakupata.

Maana ukikaa sehemu kwa muda mrefu hata kama watu wanakupenda unaweza kukumbwa na mabaya. Mimi hili nimeona niliseme tu kwa uwazi,” alisema Rais Magufuli. “This is your time, umefanya kazi nzuri, waachie vijana ili tushughulike nao, tufukazane nao.

Kama umenisikia nielewe, kama hujanielewa….,” alisema Rais Magufuli. Upotevu wa maji udhibitiwe Kuhusu kupotea maji, Rais Magufuli alisema nchi inaweza kukopa fedha nyingi, lakini asilimia kubwa ya mapato hayo yanaweza kupotea kwa maji yanayopotea.

Aliwaomba watendaji wa wizara hiyo kuhakikisha hakuna maji yanayopotea. Alisema Wizara ya Maji na Umwagiliaji wamefanya kazi nzuri, licha ya kuwa kazi zao hazionekani. “Dawasa na Dawasco tembeeni vifua mbele kwani mnafanya kazi kubwa.

Nimeiona kazi nzuri na ya kufurahisha,” alisema Magufuli. Aliwahakikishia kuwa serikali iko pamoja nao na akawataka miradi ambayo haijakamilika ukiwemo wa Lindi, wajipange na ikiwezekana Dawasa wahamie wote Dawasco wakausimamie ili uweze kukamilika.
Alisema anafahamu kuna utata kati ya Dawasa na Dawasco. “Nafahamu kuna contradiction (mkanganyiko) kati ya pande hizo mbili kati ya Dawasco na Dawasa.

Dawasco wanahoji kwa nini
Dawasa wakimaliza kufanya kazi kwa nini wasijiunge pamoja na Dawasco kufanya kazi pamoja, lakini Dawasa nao wanauliza kwa nini tusibaki na miradi hii ili tuiendeshe sisi, kwa nini tunawapa Dawasco?

Hili naliacha kwa Wizara ya Maji,” alieleza Dk Magufuli. Aagiza kukata maji Rais Magufuli pia aliiagiza wizara kuhakikisha taasisi zake zinawakatia maji taasisi zote za serikali ambazo zinadaiwa kiasi hicho cha Sh bilioni 40.

Alisema wizara hiyo ifanye uhakiki wa madeni hayo na wapeleke Wizara ya Fedha na Mipango taasisi zote zinazodaiwa ili fedha hizo zikatwe huko huko. “Na nyinyi pia lipeni shilingi bilioni nane mnazodaiwa za umeme, lakini msipofanya hivyo pia nitaiagiza Wizara ya Fedha ikate huko huko,” alisema.

Aliongeza: “Tumezoea kudekezana, maana wizara ina bajeti na fedha za matumizi zinapelekwa, lakini vipaumbele vyao vinakuwa safari za nje na semina na wanacha kulipia maji.”

Kisarawe ipatiwe maji
Aliagiza wizara kuhakikisha kuwa wanafikisha huduma ya maji katika mji wa Kisarawe ili nao wafaidike na huduma ya maji kwa kuwa nao wamekuwa wanatunza vyanzo vya maji.
Aliwataka wahandisi wa wizara hiyo kusahau yaliyopita; badala yake sasa watumie elimu zao kuwahudumia wananchi. Rais Magufuli aliwaagiza wizara na taasisi zao wakapunguze makongamano na semina ili wakafanye kazi.

“Semina zenu hizi naziorodhesha… bodi zikasimamie kazi…lakini pia hakuna haja ya kuwa na bodi nyingi ya Dawasco na Dawasa, kwa nini tusiwe na bodi moja inayosimamia maji?” alihoji.

Katibu ataja miradi saba Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Emmanuel Kalobelo alisema mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu ni miongoni mwa miradi saba ya kimakakati ambayo inalenga kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na miji ya Kibaha, Mlandizi na Bagamoyo.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini, upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, uchimbaji wa visima virefu vya Kimbiji na Mpera, ujenzi wa bwawa la Kidunda, upanuzi wa mtandao wa usambazaji maji katika meneo yote yanayohudumuiwa, kupunguza upotevu wa maji na uboreshaji wa mfumo wa mitandao ya majitaka.

Alisema miradi hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka ujazo wa lita milioni 300 hadi lita milioni 750 kwa siku ifikapo mwaka 2020. Balozi wa India, Sandeep Arya alisema tangu Waziri Mkuu wa India, Narenda Modi alipofanya ziara yake nchini, hatua mbili zaidi zimepangwa katika ushirikiano baina ya hizo mbili ikiwemo kusainiwa kwa mkataba mwezi uliopita kwa ajili ya upanuzi wa usambazaji wa maji katika miji ya Tabora, Nzega na Igunga.



Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link