MHE. MCHENGERWA AJA NA MAPINDUZI MAKUBWA KWENYE SANAA NA MICHEZO
Na. John Mapepele- WUSM
Waziri
wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohammed Mchengerwa amesema
Wizara yake itahakikisha inafanya kazi kuanzia ngazi ya mitaa na vijiji
ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta hizo katika kipindi kifupi.
Mhe.
Mchengerwa ametoa kauli hiyo usiku wa ( Januari 14, 2022) kuamkia leo
akiwa Mgeni Rasmi kwenye fainali za mashindano ya sanaa ya Bongo Star
Search (BSS) msimu wa 12 jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na
Katibu Mkuu wake, Dkt. Hassan Abbasi, na Naibu Katibu Mkuu, Said Yakubu.
"Tunataka
tuizungumze sanaa katika kila mtaa, tutaizungumza Sanaa katika kila
kata, tutaizungumza Sanaa katika kila wilaya, na tutaizungumza Sanaa
katika kila mkoa, tunataka Sanaa ndiyo iwe msingi katika kulinda na
kuendeleza utamaduni wa taifa letu" amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amesema
kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanakwenda
kufanya mageuzi katika sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Aidha,
amesisitiza kuwa yeye ni mtu wa kasi katika utendaji na matokeo zaidi
hivyo atahakikisha kuwa matokeo makubwa yanapatikana katika Wizara
yake.
Mhe. Mchengerwa amemwagiza Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi kuona uwezekano wa kuwaendeleza
washiriki wote wa shindano hilo katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo kilicho
chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Katika
mashindano hayo mshindi wa kwanza ni Bryson Yohana kutoka Dar es
Salaam, mshindi wa pili ni Andrew Charles kutoka Mwanza na mshindi wa
tatu ni Suleiya Abdi mwanadada kutoka mkoa wa Dodoma.