Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleimani Abdulla
akizungumza na waumini wa Masjid Tayyib ulipo Fuoni Kituo cha Polisi Wilaya ya Magharibi B Unguja |
Waumini wa dini ya Kiislamu wametakiwa kutumia misikiti kwa kujenga jamii bora na isiwe tu kwa kufanya Ibada pekee.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo alipojumuika na waumini wa Masjid Twayyib uliopo Fuoni kituo cha polisi Wilaya ya Magharibi "B" unguja katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Amesema jamii tulionayo inahitaji malezi zaidi hasa ya kumjua mola wao ambapo kwa kufanikiwa katika suala hilo kutaweza kusaidia zaidi kupunguza matendo maovu katika jamii, kama vile ya ubakaji, madawa ya kulevya pamoja na udhalilishaji kwa wanawake na watoto.
Amesema umefika wakati wa kurudi katika mila, silka na tamaduni za kizanzibari za kulea kwa pamoja na kukemea tabia ya wizi hasa katika sehemu za Ibada na kueleza kuwa asilimia kubwa ya wanaofanya matendo hayo wameathirika na matumizi ya madawa ya kulevya.
Mhe. Hemed amesema Serikali inategemea nguvu kazi ya vijana katika kuleta maendeleo hasa kutumika katika kujenga miradi ya mbali mbali ya maendeleo ambayo Serikali ya Awamu ya Nane imeipanga katika kuwaletea huduma bora za kijamii wananchi wake
Mhe. Hemed ameitaka Jamii kuendelea kuwa wamoja hasa panapotokea hitilafu za kukosana kibinadamu kwa kushirikiana na kuondoa tofauti hizo, ili kuweza kupata jamii yenye umoja na mshikamano baina yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ni jukumu la kila mmoja kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum wakiwemo watu wenye ulemavu, Mayatima, wajane na Maskini ili kuendeleza utamaduni uliokuwepo miaka iliyopita katika visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Akitoa Khutba Mskitini hapo Ustadh Mahmoud Abeid Hamid amewakumbusha waumini wa Dini ya Kiislamu kuacha tabia ya kudhulumu nafsi zao kwa kisingizio cha maisha kuwa magumu ,na kuamini kuwa Allah ndie mtoaji wa Riski.
……………………………
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
14/01/2022