Na Paschalia George, Afisa Habari Ilemela
Waziri
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari Mhe. Nape Nnauye (Mb)
amefungua mafunzo kwa njia ya mkutano wa video “video
conference”yanayohusu mfumo wa utambuzi wa kaya na maeneo mbalimbali wa
anwani za makazi na postikodi Tanzania.
Mafunzo
haya yanafanyika kikanda ambapo mikoa mitatu kwa Tanzania baraTanga
,Mbeya na Ilemela –Mwanza ni wenyeji sambamba na Zanzibar kwa upande wa
Tanzania visiwani.
Akizungumza
wakati wa mkutano huo Mhe. Nape amesema serikali ya awamu ya sita ya
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu inaendelea
kutekeleza miradi ya kipaumbele ikiwemo mradi huu wa anwani za makazi.
“Nataka mradi wa anwani za makazi na postikodi ukaweke alama nchini kwa utekelezwaji wake wa viwango stahiki.Nitoe rai kwa yeyote mwenye mpango wa kukwamisha zoezi hili atupishe mapema atuache tutimize azma yetu njema kwa taifa letu” amesema Mhe.Nape.
Mhe.Nape
ameongeza kuwa ni hitaji la serikali kuwa na mfumo huu ambao ni muhimu
sana kwa jamii na serikali katika kupanga mipango ya kimaendeleo ya
kiserikali sambamba na urahisi wa utoaji huduma mbalimbali za
kijamii,kufungua masoko ya biashara za mtandaoni zenye tija na kama
utatumika ipasavyo mfumo huo utaimarisha usalama na kuleta ajira zaidi
kwa jamii yetu.
Nae Mkuu
wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Hassan Elias Masala ambayo ndio wilaya wenyeji
wa mafunzo haya kwa mkoa wa Mwanza amesema amepokea zoezi hilo
kikamilifu na kuwahakikishia ulinzi na usalama wataalam wote
wanaoshiriki zoezi katika kata zote 19 zinazounda manispaa ya Ilemela
ambapo kata 4 kati ya hizo zitatumika kwa mafunzo ya vitendo kwa
washiriki wote wa mafunzo haya kutoka mikoa 8 ya jirani.