Home » » WAZIRI NDEJEMBI AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KURIDHIKA NA MISHAHARA YAO KUEPUKA VITENDO VYA RUSHWA NA UBADHIRIFU

WAZIRI NDEJEMBI AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KURIDHIKA NA MISHAHARA YAO KUEPUKA VITENDO VYA RUSHWA NA UBADHIRIFU

Written By CCMdijitali on Monday, January 17, 2022 | January 17, 2022

Waziri Ndejembi  akizungumza na Watumishi wa Manispaa ya Wilaya Sumbawanga mkoani Rukwa

 Watumishi wa Manispaa ya Wilaya Sumbawanga mkoani Rukwa


NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amesema hakuna kipindi kizuri kwa watumishi wa umma kama hichi kilichopo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan huku akiwataka watumishi wa umma kuepuka vitendo vya rushwa, ubadhirifu na kuridhika na mishahara yao.

Ndejembi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Manispaa ya Wilaya Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo amefika kusikiliza changamoto zao na kuzitatua lakini pia akitumia nafasi hiyo kuwaasa watumishi wa umma kuwa wazalendo na wenye kulisaidia Taifa lao.

Amesema ni jambo la aibu kuona mtumishi wa umma aliyeaminiwa na kulipwa mshahara kwa Kodi za watanzania akiomba rushwa ya fedha na wengine hadi ya ngono ili waweze kumsaidia mwananchi anaetaka huduma.

” Haiwezekani kila Mwananchi anaekuja kwenye Ofisi za Umma wewe mtumishi uliyepewa dhamana ndo unakua wa kwanza kuomba rushwa, wengine utasikia andika namba yako ya simu, hapo unataka rushwa ya ngono, wengine anataka kuminyiwa pesa kidogo ndio atoe huduma, niwaase watumishi wenzangu kuachana na vitendo hivyo mara moja.

Lakini pia nisisitize utoaji huduma bora tuepuke Ile dhana kwamba Watumishi wa Serikali hawana kauli nzuri kwa wateja, Mtu anaogopa kwenda kujifungulia Hospitali ya Serikali kwa kuwa wauguzi wake wana matusi, toeni huduma bora zitakazowaridhisha wananchi wetu,” Amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii kwa kutoa huduma bora, kuepuka vitendo vya rushwa pamoja na kuongeza kiwango cha makusanyo kwani kufanya hivyo kutachangia wao kuongezwa mishahara badala ya kudai ongezeko la mishahara ilihali wao wenyewe hawasaidii ukuaji wa uchumi.

” Sisi kama watumishi wa umma tunapaswa kuongeza bidii katika makusanyo, tuongeze mapato ya Serikali, kwa kufanya hivyo tunampa moyo Rais Samia wa kufikiria kutuongeza mishahara, lakini siyo sisi tunakua vinara wa rushwa halafu tunadai mishahara mikubwa, niwasihi kubadilika,” Amesema Ndejembi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Sebastian Waryuba amemuhakikishia Naibu Waziri Ndejembi kuwa Ofisi yake itahakikisha inasimamia maelekezo yote aliyoyatoa kwa watumishi ikiwemo kuboresha kiwango cha utoaji huduma, kudhibiti mianya ya rushwa sambamba na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link