Home » » MAKAMISHNA WASAIDIZI WA ARDHI NCHINI WATAKIWA KUWAJIBIKA KUFIKIA MALENGO - WAZIRI MABULA

MAKAMISHNA WASAIDIZI WA ARDHI NCHINI WATAKIWA KUWAJIBIKA KUFIKIA MALENGO - WAZIRI MABULA

Written By CCMdijitali on Friday, February 25, 2022 | February 25, 2022

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa mkoani Arusha Tarehe 25 Februari 2022.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akizungumza kwenye kikao kazi cha Menejimenti  na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa mkoani Arusha Tarehe 25 Februari 2022.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela akizungumza kwenye kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa mkoani Arusha Tarehe 25 Februari 2022.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi akizungumza katika kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa mkoani Arusha Tarehe 25 Februari 2022.

WAZIRI DKT MABULA ATAKA UWAJIBAKI KWA MAKAMISHNA WA ARDHI KUFIKIA MALENGO YA WIZARA

Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Makamishna Wasaidizi wa Ardhi wa mikoa nchini kuwajibika na kutumia wajibu wao katika kutekeleza mikakati ya Wizara kufikia malengo.

Aidha, amewataka Makamishna hao kuwapangia majukumu kwa malengo maafisa walio chini yao na kufuatilia kazi wanazowapa mara kwa mara.

Dkt Mabula amesema, hayo tarehe 25 Februari 2022 wakati akifungua kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha.

‘’Yapo malalamiko ya lugha zisizofaa kwa wateja, hii haikubaliki fuatilieni hili na kulikemea vikali na kuzingatia misingi na kanuni za utumishi wa umma katika majukumu yenu ya kila siku ’’ alisema Dkt Mabula.

Aidha, aliwataka katika utekelezaji mpango mkakati wa wizara wanazingatia vipaumbele vya serikali hususan maelekezo ya mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

Akigeukia suala la makusanyo ya kodi ya pango la ardhi, Waziri wa Ardhi aliwataka Makamishna wa ardhi Wasaidizi wa mikoa kuwa wabunifu katika njia za kukusanya mapato.

‘’Sula la mtandao kutopatikana muda mwingi linaonekana kuwa kikwazo katika ukusanyaji maduhuli, lifanyieni kazi’’ alisema Dkt Mabula.

Waziri Dkt Mabula pia alihimiza kuongezwa kwa kasi ya umilikishaji ardhi kwa wananchi na kuwataka Makamishna hao na wakuu wa idara kuweka malengo kwa kila ofisa mwenye taaluma ya ardhi kuandaa hati.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi alisema, baada ya kuteuliwa katika nafasi ya Katibu Mkuu alifanya ziara kwa baadhi ya mikoa na kubaini changamoto kadhaa alizozitaja kuwa ni pamoja na kutofikiwa malengo ya ukusanyaji kodi ya ardhi pamoja na baadhi ya halmashauri kutohudumia idara za ardhi kwa madai ya idara hizo kuhamishiwa wizarani.

‘’Nimeanza kuchukua hatua ili kutatua changamoto hizo ambapo tayari nimetoa maagizo mbalimbali kwenye mikoa na menejimenti ya wizara na ni matarajio yangu kikao kazi hiki kutaibua suluhisho la changamoto hizo’’ alisema Dkt Allan Kijazi.

Kwa mujibu wa Dkt Kijazi, Wizara ya Ardhi imekuwa ikinyooshewa vidole na wananchi kwa masuala ya ukiukwaji wa haki za wananchi na kuchafua taswira ya Wizara na kutaka watendaji wa sekta ya ardhi kujitafakari na kujisahihisha kwa kutimiza wajibu ili kuondoa dhana hiyo.

Aligusia pia mpango wa urasimishaji makazi holela na kueleza kuwa, ni matarajio yake kupitia kikao hicho, washirikia wake wataibuka na mkakati wa uelekeo wa wizara katika kupanga miji sambamba na usimamizi wa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 50 zilizotolewa kwa ajili ya mpango wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi maarufu kama KKK.

-------------------------------------------MWISHO-------------------------------

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link