Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson kwa jitihada anayoendelea kuionesha katika kuliongoza Bunge kwa maslahi ya Taifa
Mhe. Hemed Ametoa kauli hio alipofanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Tulia Ackson alipofika kujitambulisha kwa mara ya kwanza tokea achaguliwe kushika nyadhifa hiyo Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar
Mhe Hemed amesema Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan ina Imani kubwa sana na utendaji kazi wake ndani na nje ya Bunge anaoendelea kuionyesha kwa maslahi ya Watanzania.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemuhakikishia Spika huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt Hussein Ali Mwinyi itatoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kufanya kazi zake kwa ufanishi na kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wa taifa hili.
Mhe Hemed amesema kuwa Muhimili wa Bunge ni muhimu ambao una uwakilishi wa watanzania wote hivyo ana Imani Muhimili huo utasimamia Kanuni na Sheria zilizopo ili kulinda maslahi ya wananchi.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa kwa ushirikiano uliopo baina ya Spika huyo na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bunge litabaki kuwa salama na kuweza kufikia lengo la Serikali la kuwatumikia wananchi kupitia Wabunge hao liweze kufikiwa.
Kwa upende wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Bunge analoliongoza lina mashirikiano ya karibu na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ili kuwaletea maendeleo Wananchi ya Tanzania
Dkt Tulia amesema kuwa Bunge lipo tayari kupokea maelekezo yanayotolewa na Viongozi Wakuu wa Nchi ili kufikia malengo waliojipangia ya kuwahudumia wananchi walio wachagua ambao wana matumaini makubwa kupitia chombo hicho cha kutunga na kubadilisha Sheria kwa maslahi ya watanzania kwa ujumla.
……………….
Ali Moh’d Shaban
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/02/2022