📸Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema tafiti zinaonesha samaki na dagaa wanaopatikana katika Ziwa Victoria hawajaathirika kwa zebaki.
Amesema
hayo bungeni jijinin Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalumu, Mhe. Juliana Masaburi aliyetaka kufahamu iwapo Serikali
imefanya utafiti kuhusu samaki hao iwapo wameathiriwa na kemikali hiyo
kama inavyodaiwa.
Dkt.
Jafo alisema kuwa wataalamu wanaendelea kuhakikisha matumizi mbalimbali
ya kemikali hiyo katika maeneo ya Kanda ya Ziwa yanadhibitiwa huku
akiwataka waendelee kuzingatia masuala mahsusi ya kimazingira ili
kulinda nchi yetu.
Pia,
akijibu swali kuhusu udhibiti wa uchafuzi pembezoni mwa Ziwa Victoria
ambao unapunguza samaki kuzaliana hivyo shughuli za uvuvi kudorora,
waziri huyo alisema Serikali imeandaa Kanuni, Miongozo na kuhakikisha
Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) inafanyika kwa miradi ya
maendeleo iliyopo na inayotarajiwa kufanyika pembezoni mwa ziwa hilo.
Aliongeza
kuwa imeandaliwa mikakati pamoja na kuendelea kutekeleza katazo la
matumizi ya mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa ambayo kwa
kiasi kikubwa ilikuwa ikichangia uchafuzi pembezoni mwa Ziwa Victoria.
Hata
hivyo, Dkt. Jafo alibainisha kuwa uchafuzi wa mazingira unaofanyika
pembezoni mwa ziwa unatokana na shughuli za kibinadamu zisizozingatia
hifadhi ya mazingira zikiwemo utiririshaji wa majitaka kutoka katika
maeneo ya makazi pamoja utupaji wa taka ngumu kutoka majumbani na
viwandani.
Alitaja
shughuli zingine kuwa ni kilimo kisicho endelevu kinachosababisha
uchafuzi wa maji kutokana na kuongezeka kwa tabaki (segments) na
matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu na mbolea za viwandani na uchimbaji
wa madini usio endelevu.