Na Eleuteri Mangi, WUSM Dar es salaam
Serikali
kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na wasanii wa
kike wa muziki nchini chini ya Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Dada Hood
inayojishughulisha na kupinga unyanyasaji wa kijinsia na kuendeleza
sanaa wameandaa Tamasha la kuichangia Timu ya Taifa ya wanawake “Twiga
Stars,” katika kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2022.
Akizungumza
na waandishi wa habari Februari 23, 2022 jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa taasisi hiyo Mkuwe Issale (Mammy
Baby) katika mkutano wa pamoja na Kaimu Katibu Mtendaji wa BMT, Neema
Msitha, amesema tamasha hilo litafanyika Machi 8, 2022 katika Ukumbi wa
Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC).
"Siku
hiyo tumeipanga makusudi kwa kazi tatu ambazo ni kufanya harambee
kuichangia timu ya wanawake Twiga Stars, kuzindua albamu yenye nyimbo za
wasanii wa kike nchini ‘The Orange' na kuonesha vipaji vya wanawake
katika tasnia ya muziki" amesema Mkuwe.
Aidha,
Mkurugenzi huyo amesema taasisi yake imekuja na ubunifu huo kwani
inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia
Suluhu Hassan kwenye sekta za Sanaa na Michezo na juhudi za kupigania
usawa wa jinsia.
Tamasha hilo litapambwa na burudani ya wasanii wa kike zaidi ya 10.
Kwa
upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha amewapongeza
Dada Hood kwa kazi zao za kuwainua watoto wa kike hasa nia yao ya
kuichangia timu ya wanawake ya Taifa Twiga Stars.
Neema
ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kuendelea
kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusaidia sekta ya michezo kwa
upande wa timu za taifa za wanawake ambazo zinaendelea kupeperusha vema
bendera ya taifa kimataifa.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Bi Leah Kihimbi amesema
Rais Samia anapenda Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo na taasisi ya
Dada Hood ndiyo wamefungua milango ya mashirikiano na sekta binafsi na
Serikali kwenye sekta za Sanaa na Michezo na kuzitaka taasisi nyingine
kuiga mfano huo kwa maslahi mapana ya taifa.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake (TWFA),
Somoe Ng'itu ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Dada
Hood na kuwakaribisha wadau wengine kuendelea kuwashika mkono Twiga
Stars kwa niaba ya mabinti wengine michezoni kwani wanafanya vyema sana
kimataifa ili waendelee kuliheshimisha Taifa.
Katika
kikao hicho na waandishi wa habari, Taasisi ya Dada Hood pia imesaini
Mkataba wa kusambaza album ya The Orange na kampuni ya Slide Visual
ambapo sehemu ya mapato yatakayopatikana na yale ya harambee yatasaidia
juhudi ya kupigania usawa wa jinsia, kuondoa ukatili kwa wanawake na
kusaidia Twiga Stars.