Waziri ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt Allan Kijazi
WIZARA YA ARDHI YATOA SIKU 60 WENYE VIWANJA VILIVYOPIMWA KUWASILISHA MAOMBI YA KUMILIKISHWA
Na Munir Shemweta, WANMM
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa siku 60 kuanzia tarehe 5 Februari 2022 kuhakikisha wamiliki wa ardhi waliopimiwa viwanja kuwasilisha maombi ya kumilikishwa ardhi huku wale wenye miliki za ardhi wawe wamelipa kodi ya pango la ardhi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo tarehe 4 Februari 2022, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na ,Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi alisema, mmiliki ambaye hatalipa kodi ndani ya muda uliotolewa, Serikali itachukua hatua za kisheria ikiwemo kufuta miliki, kupiga mnada na kumilikisha viwanja vilivyopimwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji.
‘’Mmiliki ambaye hatalipa kodi ndani ya muda uliotolewa Serikali itachukua hatua za kisheria ikiwemo kufuta miliki, kupiga mnada na kumilikisha viwanja kwa wananchi wenye uhitaji, hatua hizi zitaanza kuchukuliwa tarehe 6 April 2022’’ alisema Dkt Kijazi .
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ni wajibu wa kisheria kwa wamiliki amabao ardhi zao zimepangwa na kupimwa kuwasilisha maombi ya kumilikishwa ardhi kwa Kamishna wa Ardhi ili kumilikishwa sambamba na kulipa kodi ya pango la ardjhi.
‘’Ni wajibu wa kisheria kwa wale wamiliki wa ardhi ambao ardhi zao zimepangwa na kupimwa kuwasilisha maombi ya kumilikishwa ardhi kwa Kamishna wa Ardhi kwa ajili ya kumilikishwa na kulipa kodi ya pango la ardhi’’ alisema Dkt Kijazi.
------------------------------