CHUO KISHIRIKI MKWAWA
CHASHAURIWA KUTANGAZA FURSA ZA
SHAHADA ZA UMAHIRI
Na WyEST,
IRINGA
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) ameushauri uongozi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kujikita kutangaza fursa hasa za Shahada za Umahirii ili kuongeza mapato ya ndani ya chuo hicho.
Ameyasema hayo mkoani Iringa mara baada ya Kamati hiyo kukagua Mradi wa ujenzi wa Maabara ya Kemia na ya Viumbehai zinazojengwa katika chuo hicho na kuongeza kuwa mapato hayo yanaweza kutumika kujenga mabweni yatakayosaidia kupunguza changamoto hiyo.
"Nimeona katika taarifa yenu mna idadi ndogo ya wanafunzi wa Shahada za umahiri, inabidi mfanye jitihada kubwa kukitangaza chuo hasa katika Shahada hizo ambazo zina idadi ya wanafunzi wachache ili kujiongezea mapato ya ndani," amesema Mhe. Nyongo.
Katika hatua nyingine Mhe. Nyongo pia ameitaka Wizara ya Elimu kufuatilia suala la kukiboresha kukipandisha hadhi Chuo cha Ualimu Mtwara ili kitumike kuzalisha walimu watakaofundisha katika Shule za Sekondari nchini.
"Tumejenga shule nyingi kipindi hiki na tuna upungufu wa walimu, nashauri Wizara ifuatilie suala la kuwa na Chuo Kikuu katika mkoa wa Mtwara ambalo limeshaongelewa hata bungeni ili tuweze kuzalisha walimu wengi watakaopunguza changamoto ya upungufu wa walimu katika Shule za Sekondari," amesema Mhe. Nyongo.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) amesema Wizara imepokea mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na Taasisi husika.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe amesema Serikali imepokea mkopo wa Dola milioni 425 kupitia Mradi wa HEET zitakazotumika kuboresha Vyuo na Taasisi za Umma za Elimu ya Juu ambapo Chuo cha MUCE kitapatiwa Dola milioni 8 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya chuo hicho.
@ikulu_mawasiliano @ikulu_habari @ofisi_ya_makamu_wa_rais @owm_tz @professoradolfmkenda @omarikipanga2021 @amani.sedo @daruso_muce2 @bunge.tanzania @neemalugangira @mjengwamaggid @sisi_tanzania_mpya