Mradi wa JNHPP wafikia asilimia 56
🔷Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini yapongeza
Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba ameeleza kuwa, utekelezaji wa Mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kwa sasa umefikia asilimia 56 na kwamba Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kasi, uadilifu, ubora na viwango vinavyotakiwa ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Waziri Makamba ameyasema hayo tarehe 16 Machi, 2022, Rufiji mkoani Pwani wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi huo.
Ameeleza kuwa, mradi huo kwa sasa unatekelezwa kwa kasi kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika usimamizi na uendeshaji wa mradi huo ambapo alitaja baadhi ya maboresho hayo kuwa ni kuongeza utaalam na wataalam pia Mkandarasi wa mradi huo, ambaye ni kampuni ya Elsewedy Electric amehimizwa kuongeza wataalam wenye uzoefu wa usimamizi wa miradi mikubwa kama wa JNHPP.
Ametaja maboresho mengine kuwa ni mabadiliko ya uongozi katika mradi, kubadili mfumo wa mawasiliano kati ya Wizara na TANESCO pamoja na TANESCO na Mkandarasi pamoja na mabadiliko ya Menejimenti na Bodi ya TANESCO ambayo yamekuja na mbinu za kisayansi za kutekeleza mradi huo na matunda yake yameanza kuonekana.
Ameongeza kuwa, kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita mradi ulikuwa chini ya asilimia 40 lakini sasa umefikia asilimia 56 na kwamba na kwa upande wa malipo kwa Mkandarasi, mwaka jana malipo yaliyofanyika yalikuwa ni takriban shilingi Trilioni Mbili na hadi sasa malipo yaliyokwishafanyika ni shilingi Trilioni 3.4.
Kutokana na hayo, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria katika kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa ili nchi iweze kuwa na umeme wa uhakika ambapo amekuwa akiidhinisha fedha zinazotolewa na Serikali ili kutekeleza mradi huo.
Waziri Makamba ameeleza kuwa, ujenzi wa Bwawa la umeme katika mradi wa JNHPP unaenda sambamba na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka kwenye bwawa kwenda Chalinze mkoani Pwani (km 160), kujenga kituo cha kupoza umeme Chalinze na kujenga mradi wa upanuzi wa gridi ya Taifa kwa upande wa Kaskazini