HATUTAWASHUSHA VYEO TU BALI
MTAONDOLEWA KWENYE
UTUMISHI WA UMMA’ BASHUNGWA
OR-TAMISEMI
Waziri
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent
Bashungwa amesema hatawafumbia macho watumishi ambao hawatoshi na kuwa
wataondolewa kwenye utumishi wa umma na si kuwashusha vyeo au
kuwahamisha
Pia Mhe. Bashungwa amewataka watumishi katika
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kufanya kazi kwa bidii, kujituma
na uadilifu mkubwa na kwa wachache wanaoenda kinyume na taratibu hizo
watachukuliwa hatua kwa kutolewa kwenye utumishi wa umma.
Amesema
kumekuwepo na utaratibu wa kuwashusha vyeo watumishi wachache ambao
wanafanya kazi kwa mazoea na kutozingatia taratibu za kiutumishi lakini
chini ya usimamizi wangu hilo jambo halivumiliki watatolewa kwenye
utumishi wa umma maana wanadhohofisha mchakato mzima wa kuleta maendeleo
kwa Watanzania.
Mhe. Bashungwa ametoa wito huo 29, Machi 2022
alipozungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma muda mfupi baada ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
kuiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI kuzisimamia Halmashauri ipasavyo na
kuchukua hatua kwa watumishi wenye matumizi mabaya ya fedha za Serikali.
“Nimuhakikishie Mheshimiwa Rais kwa maagizo aliyoyatoa leo kuhusu weledi na uadilifu wa Watumishi wa umma, nitaanzia hapa Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha tunajenga taswira na mwelekeo unaoendana na ofisi ya Mheshimiwa Rais” amaesema Bashungwa
Amesema matarajio yake ni kuona wale wachache waliokuwa wanaenda kinyume wanabadilika na kujirekebisha maana kuna Watanzania wasomi na wazalendo wapo mtaani ambao wakipewa nafasi wataweza kutumikia Watanzania kwa uaminifu.
Aidha, Waziri Bashungwa amemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI ndani ya siku tatu kuhakikisha anamaliza uchambuzi wa Wakahazina wa Halmashauri ambao hawafanyi kazi kikamilifu ili waweze kuchukuliwa hatua.
Pia, Waziri Bashungwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia nidhamu ya Utumishi katika maeneo yao hasa katika usimamizi wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuchukua hatua mapema kabla ya Wizara haijalazimika kufanya hivyo.