Na Waandishi Wetu, Dar
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) imeipongeza
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa juhudi
ilizozichukua hadi kufanikisha zoezi la kuwarejesha salama wanafunzi
waliokuwa nchini Ukraine.
Pongezi
hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Vita Kawawa (Mb)
Jijini Dar es Salaam wakati Kamati hiyo ilipotembelea Chuo cha
Diplomasia (CFR).
Katika
Kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula pamoja na
Naibu Katibu Mkuu Mhe. Balozi Fatma Rajab.
“Nichukue
nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Wizara kwa jinsi mlivyoshughulikia
suala zima la kuhakikisha wanafunzi wa Kitanzania walioko nchini Ukraine
wanarejea salama nchini,” amesema Mhe. Kawawa.
‘’Mhe.
Waziri tunawapa pongezi nyingi, kwa kazi na hatua kubwa mlizochukua
na jinsi mlivyoshirikiana na wazazi wenye wanafunzi waliokuwa wanasom
nchini Ukraine hasa ikizingatiwa kuwa wazazi hao waliwapeleka watoto wao
binafsi bila ya kuishirikisha Serikali,’’ ameongeza Mhe. Kawawa.
Amesema
kamati imeridhishwa na jinsi ambavyo Wizara ilivyosimama imara na
kuwasaidia Watanzania wote waliokuwepo nchini Ukraine na kuhakikisha
wanarejea nyumbani salama.
Mhe.
Kawawa ametoa wito kwa Watanzania wanapokuwa nje ya nchi kujiandikisha
katika Balozi za Tanzania ili kuwa rahisi kuwaratibu pale inapotokea
athari yoyote kule wanapokuwepo.
Mhe.
Kawawa amewapongeza vongozi wa wizara, mabalozi na watumishi wa wizara
ambao kwa namna moja au nyingine wamefanikisha uondoaji wa watanzania
waliokuwepo nchini Ukraine.
Akizungumza
katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameihakikishia kamati hiyo kwamba
Uongozi wake utaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na
kuhakikisha inasimamiwa ili ikamilike kwa wakati na kuendana na thamani
halisi ya fedha iliyotolewa na Serikali.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea Chuo Cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam |
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Stella Ikupa akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea Chuo Cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam |