SHIRIKA LA POSTA, KAMPUNI YA NDEGE ZA TANZANIA ZASAINI MKATABA WA KIBIASHARA
Prisca Ulomi, WHMTH, DSM
Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) zimesaini mkataba wa
kibiashara leo wa kuziwezesha taasisi hizo za umma kusogeza huduma zake karibu kwa
wananchi.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameshuhudia
hafla hiyo ya utiaji saini mkataba baina ya taasisi hizo mbili ya TPC na ATCL na kuzindua rasmi
ushirikiano huo wa kibiashara ambapo TPC kama wakala wa ATCL imemkatia tiketi ya ndege
ya ATCL Waziri Nape papo hapo baada ya uzinduzi huo
“Niwapongeze kwa ubunifu mkubwa mliofanya, na hii imechagiza maono ya Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan ya kufikisha huduma kwa wananchi na muwahamishe wananchi kutumia
huduma hizo”, amesema Waziri Nape
Waziri Nape ameongeza kuwa, “ATCL mna mashirika ya ndege mnayofanya nayo kazi, na TPC
nao wana mashirika yao huko duniani, hivyo ATCL na TPC wote mtanufaika ni vizuri
mkashirikiana na sekta binafsi, acheni kujifungia, tokeni nje, mnachokipata mtagawana na
kuongeza tija ya mashirika yenu “.
“ATCL na TPC mkawajibike ipasavyo ili huduma zote za mashirika haya ziwe nzuri zaidi na
ubora wa huduma uzingatiwe, hivyo msifumbiane macho, mwambizane ukweli kwa kuwa
unapomkamua mtu jipu atapiga kelele ila kesho atapona; ubora wa huduma zenu utavutia
sana wateja,” amesisitiza Waziri Nape
Akizungumza wakati anamkaribisha Waziri Nape, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,
Mohammed Khamis Abdulla amesema kuwa ajenda kuu ya Wizara hiyo ni kuipeleka Tanzania
Kidijitali na mashirikiano baina ya TPC na ACTL ni moja ya njia ya kuifikisha nchi Kidijitali huku
akiugusia mfumo wa anwani za makazi kama njia nyingine ya kuipeleka Tanzania Kidijitali
“TPC inategemea usafiri wa haraka, salama na unaoaminika na ATCL inahitaji kufikia wateja
wake, hivyo ushirikiano huu ni muhimu,” amesema Abdulla
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Brigedia Mstaafu Yohana Mabongo amesema kuwa bodi
itahakikisha ndoa baina ya ATCL na TPC inashamiri ili nchi yetu itoboe katika ya uchumi kwa
kuhakikisha kuwa ushirikiano wa kibiashara uliosainiwa leo hii unaenda kuhudumia wananchi
ipasavyo
Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo amesema kuwa TPC
imeona fursa ya kutumia ATCL kuwa wakala na kufanya makubaliano ya kibiashara ikiwemo
wakala wa kukata tiketi za ndege na usafirishaji wa vifurushi kwa kuwa TPC ina matawi zaidi ya
350 nchi nzima hivyo TPC itasogeza huduma kwa wananchi
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladslaus Matindi amesema kuwa tukio hili ni kubwa
kwa ATCL kwa kuwa wameangalia namna mpya ya kufanya biashara na TPC na kutumia fursa
hii kwa kuwa TPC ni Shirika pekee lenye mtandao mpana mpaka vijijini ambao ni sawa na
ilivyo vituo vya afya na shule zilivyo kila mahali na fursa hii itawanufaisha wote ATCL na TPC
kwa kuwa kwa sasa dunia ni kama Kijiji.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari