SERIKALI KUBORESHA UPATIKANAJI WA
HUDUMA ZA DAWA NCHINI
Serikali
kupitia Wizara ya afya imejipanga kukabiliana na ukosefu wa dawa muhimu
katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini.
Hayo
yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu mbele ya Kamati ya
kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii wakati akiwasilisha
randama ya bajeti ya Wizara mwaka wa fedha 2022/2023.
Waziri
Ummy amekiri kuwa na uhaba wa dawa katika vituo vingi vya kutolea huduma
za afya nchini huku sababu ikitajwa kuwa ni kutozingatia mpango kazi wa
manunuzi ya dawa pamoja na matumizi na usimamizi katika ngazi za vituo
vya kutolea huduma za afya.
“Maoteo ya dawa yanatakiwa kuletwa
Wizarani kutoka katika vituo vya kutolea huduma, tumeshaonesha magonjwa
kumi yanayoongoza nchini hivyo inatakiwa kila kituo kijue ni magonjwa
gani yanayoongoza kwa wananchi wa eneo hilo. Hivyo kituo kiweke mpango
kazi wa manunuzi pamoja na matumizi sahihi ya dawa ili kuepusha
kukosekana na kupelekea kero kwa wananchi”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri
Ummy ameongeza kuwa ni jukumu la Mganga Mkuu wa Wilaya kupitia maoteo
yanayoletwa kutoka katika vituo kama ni sahihi yaende ngazi ya mkoa na
kisha Wizarani. Hatua hii itasaidia wizara kupanga bajeti ya dawa ambayo
itakidhi mahitaji ya nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa afya
Dkt. Godwin Mollel amesema mfumo wa ununuzi wa dawa katika bohari ya
dawa (MSD) bado unaleta changamoto kwenye vituo vya kutolea huduma
ambapo dawa zinapoagizwa hazifiki kama mahitaji yanavyotaka.
Dkt.
Mollel amesema hali hii husababisha ukosefu wa dawa katika vituo na
kuwafanya watoa huduma kuwaandikia wagonjwa fomu za kwenda kununua
katika maduka binafsi.
Ili kutatua changamoto hiyo pamoja na
nyingine Waziri Ummy aliiomba kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na
maendeleo ya jamii kupitisha bajeti ya Shilingi Trilioni 1.109 kwa ajili
ya uendeshaji wa Wizara ya Afya ambapo wajumbe wa kamati wakiongozwa na
Makamu Mwenyekiti Mhe. Aloyce Kamamba ilipitisha na kuwa bajeti rasmi
ya mwaka 2022/2023.