Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutoa fursa kwa vijana nchini ili waweze kuondokana na changamoto ya ajira.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo Machi 19, 2022 alipoambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea mradi wa Kitalu Nyumba (Greenhouse) katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru kwa lengo la kukagua maendeleo ya mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Amesema kuwa, katika kufanikisha hilo Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiratibu Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo imelenga kuwezesha nguvu kazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili kumudu ushindani wa soko la ajira na kuwawezesha kujiajiri au kuajiri wenzao.
“Mheshimiwa Rais amedhamiria kutoa fursa zaidi kwa vijana nchini na serikali anayoiongoza imekuwa ikiwapatia vijana fursa mbalimbali ikiwemo ujuzi na stadi za kazi ili waweze kushiriki kwa ufanisi katika shughuli za uzalishaji mali sambamba na kuongeza fursa za ajira,” alisema Waziri Ndalichako
Aliongeza kuwa, Serikali imetenga shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kupitia mafunzo ya uanagenzi, mafunzo ya utarajali (Internship Training), mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana katika mfumo usio rasmi wa mafunzo na mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia kitalu nyumba (Greenhouse Farming Training).
Akizungumzia mafunzo hayo ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba, alisema kuwa zaidi ya vijana 702 kutoka katika halmashauri 7 mkoani Arusha wamenufaika na mafunzo hayo ambapo vijana hao wamepatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo ya ujenzi wa kitalu nyumba pamoja na kilimo ndani ya kitalu nyumba (Greenhouse).
Aidha, Waziri Ndalichako alitoa wito kwa Viongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kuwezesha vijana vitendea kazi ili wafanye shughuli zenye tija.



