Home » » TANZANIA YAPOKEA CHANJO DHIDI YA UVIKO-19 AINA YA SINOVAC

TANZANIA YAPOKEA CHANJO DHIDI YA UVIKO-19 AINA YA SINOVAC

Written By CCMdijitali on Wednesday, March 23, 2022 | March 23, 2022






  

TANZANIA YAPOKEA CHANJO DHIDI YA

 UVIKO-19 AINA YA SINOVAC


Serikali kupitia wizara ya Afya imepokea chanjo ya UVIKO-19 aina ya SINOVAC kutoka Serikali ya Uturuki jumla ya dozi 1,000,000 kati ya dozi 4,000,000 zinazotarajiwa kupokelewa kwa awamu nne.

Chanjo hizo zimepokelewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Machi 23, 2022 katika uwanja wa ndege wa Kimatiaifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

"Kwa niaba ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan tunaishukuru Serikali ya Uturuki kwa kupokea ufadhili wa chanjo hii itakayokwenda kuwasaidia watanzania." Amesema Waziri Ummy


Hadi sasa Serikali imepokea jumla ya chanjo ya UVIKO-19 dozi 10,845,774 zikijumuisha (Sinopharm, Janssen, Moderna, Pfizer na Sinovac) ambazo zinatosha kuchanja watu 6,381,327.

Waziri Ummy amesema Serikali itaendelea kutoa chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za Afya kwa mujibu wa miongozo iliyopo.

Hadi kufikia Machi 21, 2022 jumla ya watu milioni 3,016,551 wamepata chanjo kamili kati ya watu milioni 30,740,928 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ikiwa ni sawa na asilimia 9.81.

"Nachukua fursa hii kuendelea kuwasisitiza Viongozi na watendaji wa ngazi zote kuendelea kuhamasisha umuhimu wa chanjo na wapate chanjo ili wajikinge na maambukizi ya UVIKO-19." Amesema Waziri Ummy


Aidha, katika kufikia kinga jamii ya UVIKO-19, Serikali inalenga kuchanja asilimia 70 ya Watanzania kuanzia umri wa miaka 18 hadi mwisho wa mwaka 2022.

Pia, Waziri Ummy ametoa rai kwa wakuu wa Mikoa kuongeza juhudi za uhamasishaji jamii ili kuongeza kiwango cha utoaji wa chanjo kwa wananchi.

"Vilevile, ninawaelekeza wataalamu kujumuisha huduma za chanjo ya UVIKO-19 sambamba na huduma nyinginezo za Afya zikiwemo afya ya uzazi,mama na mtoto, VVU, Tohara, Macho, Lishe, na Kifua Kikuu." Amesema Waziri Ummy

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link