WAZIRI PROF. MBARAWA AZINDUA BODI MPYA YA TPA
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameipa maelekezo
matano Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),
huku akisisitiza endapo yakifanyiwa kazi kwa usahihi taasisi hiyo,
itapiga hatua katika utekelezaji wa majukumu yake na kuleta tija
inayokusudiwa.
Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizindua Bodi hiyo
mpya jijini Dar es Salaam huku akiitaka kusimamia utendaji kazi katika
masoko, manunuzi ,uhandisi na mifumo.
Profesa Mbarawa amesema
Serikali ina imani kubwa na bodi hiyo, inayoongozwa na Mkuu wa Jeshi la
Polisi mstaafu, Balozi Ernest Mangu aliyeteuliwa hivi karibuni na Mhe.
Rais Samia Suluhu Hassan.
"Bodi iliyopita ilivunjwa kwa sababu mamlaka ya uteuzi ilikosa imani na utendaji kazi wake ikiwemo kuendelea kulea ubovu wa TPA hivyo Wajumbe wote tambueni mna majukumu makubwa na imani yangu kwenu ni kuhakikisha mnafanya vizuri ili kuleta matokeo chanya ndani ya TPA," amesisitiza Prof. Mbarawa.
Katika maelezo yake, Profesa Mbarawa alitolea mfano utendaji kazi wa bandari ya Dar es Salaam, akisema bado haujafikia kiwango kinachotakiwa, licha ya mizigo na meli zinazopakua mizigo kuongezeka kwa nyakati tofauti.
“Hakuna sababu ya msingi ya mchakato wa kupakua mizigo kuchukua muda mrefu kati ya siku 20 hadi 30, hili jambo linatakiwa kufanyiwa kazi haswa. Suala hili likisimamiwa vema litapunguza msongamano wa meli zinazoingia na kutoka", amebainisha.
Ameitaka Bodi hiyo iangalie utendaji kazi wa mtoa huduma mwenza wa TPA ambao hauridhishi na kuitaka TPA ifikishe malengo iliyojiwekea ya kukusanya mapato zaidi.
Katika mkutano huo, Profesa Mbarawa alivitaja vitengo vya idara ya manunuzi na masoko, akisema bado havijatekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku akiitaka bodi hiyo mpya kuangalia sekta hizo kwa jicho la tatu.
Amebainisha kuwa lipo soko kubwa DRC (Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo), hivyo TPA ikijipanga vizuri itanufaika na soko hilo na hivyo kuleta tija.
Aidha, kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Balozi, Ernest Mangu akizungumza amesema watajitahidi kufanyakazi kwa bidii ili kufikia lengo.
@tpa_tz



