Afisa kutoka Idara ya
tiba-Wizara ya Afya,sehemu ya kinywa na meno Dkt. Msafiri Kabulwa
WATAALAM WA KINYWA NA MENO
WATAKIWA KUTOZIBA MENO KWA
MADINI YA ZEBAKI
Na WAF Mbeya
Wizara
ya Afya kwa kushirikiana na asasi ya AGENDA imewataka wataalamu wa Afya
ya kinywa na meno kutokuziba meno bila kutumia dawa yenye madini ya
zebaki ijulikanayo kama Amalgma kutokana na kuwa na athari kwa
binaadamu.
Wito huo umetolewa leo na Afisa kutoka Idara ya
tiba-Wizara ya Afya,sehemu ya kinywa na meno Dkt. Msafiri Kabulwa wakati
wa mafunzo kwa wataalamu wa afya ya kinywa na meno juu ya kuziba meno
kwa kutumia kemikali zisizo na madini ya zebaki yaliyofanyika jijini
Mbeya.
Dkt. Msafiri amesema Zebaki ina athari kubwa kwenye
mazingira na afya ya binaadamu, pia ina uwezo wa kuharibu ukuaji wa
ubongo wa mtoto tangu akiwa tumboni kwa mama
"Zebaki huweza kutoka kwa mama mjamzito na kuingia kwa mtoto aliye tumboni wakati wa ujauzito, ama kupitia maziwa ya mama wakati wa kunyonyesha na kuleta athari katika ukuaji wa ubongo wa mtoto."Amesema Dkt. Msafiri
"Athari za ukuaji wa ubongo ni pamoja na kuharibu uwezo wa mtoto wa kufikiri na hatimaye kumfanya mtoto ashindwe kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi hapo baadaye" Amesema Dkt. Msafiri
Aidha, Dkt. Msafiri amesema wizara imelenga kuikinga jamii dhidi ya madhara yatokanayo na madini ya zebaki kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kuzibia meno zisizokuwa na madini ya zebaki kupitia bohari ya dawa(MSD)
"Kemikali za kuzibia meno zisizokuwa na madini ya zebaki zinapatikana hapa nchini kwa wasambazaji binafsi na kupitia bohari ya dawa (MSD)" Amesema Dkt. Msafiri
Naye, Afisa programu mwandamizi wa asasi ya AGENDA Bi. Dorah Swai amesema Mwaka 2013 Tanzania iliungana na nchi nyingine ulimwenguni kusaini Mkataba wa Kimataifa wenye lengo la kulinda afya na mazingira kutokana na athari za zebaki unaojulikana kama Mkataba wa Minamata wa Zebaki ambapo Tanzania iliridhia mkataba huo mwezi Oktoba 2019 na hivyo kuuzidishia nguvu ya utekelezwaji wake hapa nchini.
"Kwa sasa ni juu ya wataalam wetu kuunga mkono juhudi hizo kwa kutimiza yale yote yalioainishwa kwenye mwongozo na kwenye kanuni, endapo walikuwa hawajaanza kufanya hivyo."Amesema BI. Dorah
MWISHO