Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (kulia) akiteta jambo na Balozi wa Denmark Bi. Mette Norgaard (kushoto) katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma. |
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Denmark Bi. Mette Norgaard katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Pamoja na mambo mengine Waziri Ummy amemshukuru balozi huyo
na Serikali yake kwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya katika kuimarisha
huduma za afya ambapo Denmark inachangia katika mfuko wa pamoja wa afya (Health
Basket Fund).
Waziri Ummy amemueleza Balozi huyo kuwa kasi ya uchanjaji wa
chanjo ya UVIKO-19 nchini bado ni ndogo lakini Serikali kwa kushirikiana na
wadau inaendelea kujikita katika kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii
kuhusu kuchanja kama afua muhimu ya kujikinga na UVIKO-19 na kupunguza uwezekano
wa kwenda kwenye hali ya dharura endapo mtu atapata maambukizi ya ugonjwa huo.
Aidha, Waziri Ummy amewashukuru wadau wa maendeleo ambao
wameiletea Tanzania chanjo ya UVIKO-19 hadi kufikia tarehe 3 Aprili 2022 watu
3,318,374 wameshachanja ikiwa ni sawa na asilimia 10.79 ya idadi ya watu
Tanzania huku lengo ni kuchanja asilimia 70 hadi kufikia Desemba 2022.
Waziri Ummy amemueleza Balozi Mette kuwa Serikali inaboresha huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi kwa kuongeza watumishi wa afya, bima ya afya kwa wote, kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na magonjwa ya milipuko na namna ya kukabiliana nayo pamoja na kuboresha huduma ya mama na mtoto pamoja na masuala ya lishe.
Kwa upande wake balozi wa Denmark Bi. Mette amesema serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha huduma za afya ili ziweze kuwafikia wanachi katika maeneo yao na kuondoa changamoto ya kuzitafuta kwa umbali mrefu.