Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana |
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
BALOZI DKT. CHANA ATOA UFAFANUZI
WA ADHIMISHO LA MIAKA 100 YA
MWALIMU NYERERE
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amewasihi Watanzania wajitokeze kwa wingi katika maadhimisho ya kusherehekea miaka 100 ya Urithi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yatakayofanyika Aprili 13, 2022 Butiama mkoani Mara ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Akizungumza leo Jijini Dodoma Balozi Dkt. Chana amesema lengo la maadhimisho hayo ambayo yanafanywa na Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na mkoa wa Mara ni kuenzi na kusherekea mchango maridhawa alioutoa Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Nyanja mbalimbali kitaifa na Kimataifa
Waziri Chana ameeleza kuwa maadhimisho hayo ni moja ya sehemu ya kutekeleza mpango wa Miaka 10 wa kuenzi Urithi wa maisha ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambao unalenga kuwashirikisha wadau ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mchango wake na umuhimu wa kumuenzi Mwalimu Nyerere , kukusanya, kuendeleza, kuhifadhi na kutangaza rasilimali za urithi wa Mwalimu Nyerere kwa manufaa ya kiazi cha sasa na kijacho ili kukuza na kuedeleza utalii.
“Tarehe 13 Aprili, 1922 ndiyo siku aliyozaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kama angekuwa hai tarehe 13 Aprili, 2022 angetimiza miaka 100, hivyo tunasherehekea kuenzi Urithi wa maisha ya Hayati Baba wa Taifa ” amesisitiza Balozi Dkt. Chana
Waziri Chana amewaalika wananchi na wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwl. Julius kambarage Nyerere ambapo maandalizi ya maadhimisho hayo yanafanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Mara.
“Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Mkoa wa Mara tunawaalika wananchi na wadau wote kushiriki kwenye kilele cha maadhimisho haya vilevile kuendelea kuenzi kwa vitendo Urithi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Baba wa Taifa letu”
Aidha,amesema kuwa kuelekea kilele cha maadhimisho hayo matukio mbalimbali yanaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na mikutano ya wadau mbalimbali.