Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa nane nchini kujitathimi kutokana na kushindwa kutoa taarifa ya uhakiki wa mashamba katika muda uliopangwa.
Waziri wa Ardhi aliagiza ufanyike uhakiki wa mashamba na kupatiwa taarifa ifikapo Julai 2022 ambapo katibu mkuu aliongeza muda huo hadi Agosti 15, 2022 taarifa hizo ziwe zimewasilishwa.
Dkt Mabula alitoa kauli hiyo tarehe 6 Septemba 2022 wakati wa kikao kazi cha Makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa 26 nchini kilichofanyika jijini Dar es Salaaam.
Makimishna wa Ardhi Wasaidizi wanaotakiwa kujitathmini ni kutoka mikoa ya Arusha, Dodoma, Geita, Kagera, Njombe, Shinyanga, Simiyu na Songwe. Hadi wakati Dkt Mabula anakutana na Makamishna ni mikoa 17 pekee iliyowasilisha taarifa za uhakiki wa mashamba
Aidha, Waziri wa Ardhi ameonesha kutofurahishwa na utendaji kazi wa Makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa ya Rukwa na Simiyu na kuelekeza kuondolewa katika nafasi yake kamishna wa mkoa wa Rukwa Swagile Juma.
Pia alionesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Wizarani Bw. Venance Mworo na kuelekeza Mkurugenzi huyo kuhamishwa Wizarani kutokana na kushindwa kwenda na kasi ya ubadilishaji mifumo ya Tehama hasa ikizingatiwa wizara kwa sasa iko katika mabadiliko makubwa ya kwenda katika mifumo ya kidigitali.
‘’Mhe Rais ameelekeza kazi ziende kwa kasi kubwa na sehemu tunaingia katika mfumo wa kidigitali ambapo tumeanza katika kasi hii lakini tunaye mkurugenzi wa TEHAMA ambaye ameshindwa kuendana na kasi ya mhe Rais’’ alisema Dkt Mabula
‘’Hili haliwahusu ninyi pekee nataka ujumbe uwafikie wataalamu wote wa sekta ya ardhi kuwa tunachukua hatua ili kuhakikisha tunaimarisha utekelezaji wa malengo tuliyojiwekea’’ alisema Dkt Mabula
#ardhiyetu