Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Mawakili wote wa Serikali ambao hawajasajiliwa kwenye rejista ya Mfumo wa Taarifa wa Mawakili wa Serikali kujisajili kabla ya muda kupita ili watambulike na Mfumo wa Kieletroniki wa Taarifa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ujulikanao kwa jina la OAG-MIS.
Mhe Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali kabla ya kuzindua Chama cha Mawakili wa Serikali (Public Bar Association) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete Dodoma wenye Kauli mbiu isemayo, “Utekelezaji wa Majukumu Unaozingatia Sheria ni Nyenzo Muhimu kwa Maendeleo ya Taifa”.
“Amri inapotoka Wanasheria wajisajili na muda umetolewa kama mtu hajajisali awe na dharura ya maana sana, ama alikuwa mgonjwa hospitalini hawezi au alipokuwa hakuna mtandao hakupata taarifa kwa wakati lakini kama muda utapita na usajili hajafanya basi Mwanasheria Mkuu nakutaka kusimamia hilo”, amesema Mhe. Rais Samia
Amemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwahimiza wale ambao bado hawajajisajili wajisajili kwenye mfumo wa OAG-MIS vinginevyo baada ya muda kupita hawatatambulika kama Mawakili wa Serikali na itabidi watafute sekta za nje wajisajili au kupewa msamaha na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Rais Samia amepongeza uanzishwaji wa Chama cha Mawakili wa Serikali cha kitaaluma na kusema uwepo wake utasaidia zoezi la kuratibu utendaji kazi wa Mawakili wote wa Serikali walio katika utumishi wa umma nchini na mmepata mlezi mzuri Mwanasheria Mkuu wa Serikali anayeweza kuwasemea katika masuala yenu ya kitaaluma, kikazi, kinidhamu na kimaslahi.
“Lakini nimefurahishwa kusikia kwamba Chama hiki sasa kilichoundwa kitafanya kazi kwa karibu na Chama cha Mawakili cha Tanganyika (TLS), lakini pia nimefurahishwa na kusikia uhusiano wa karibu wa kazi baina yenu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar”, amesema Mhe. Rais Samia
Aidha, amesema itakuwa ni rahisi kuwasiliana kupitia mfumo huo wa Mawakili wa Serikali ambao ameuzindua na kusema ni dhahiri maboresho hayo yataongeza ari na tija kwa Mawakili wa Serikali wanapotekeleza majukumu yao katika maeneo mbali mbali nchini.
Akimkaribisha Mhe. Rais Samia, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema mkutano huo ulitanguliwa na kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara, Taasisi, Idara na Halmashaurizote nchi nzima na kuelezwa kuhusu mpango wa kuanzisha Chama cha Mawakili wa Serikali.
Dkt. Ndumbaro amesema chama hiki kitakuwa kikisimamia masuala ya kitaaluma na masuala ya kimaadili ya Wanasheria na ni fursa nzuri ya kutoa changamoto za kimaadili ambazo zimekuwa zikiwakabili na itawezekana tu kama Mhe. Rais Samia atakubali ombi la kuzindua chama hicho.
“Mhe Rais Samia kupitia Chama cha Mawakili wa Serikali tunatarajia kwamba chama hiki kitaleta umoja wenye nguvu na jukwaa mahususi kabisa la kuishauri Serikali katika mambo mbalimbali ya kisheria na tunatarajia kwamba itakuwa ni sehemu ya majidiliano ya kisheria kwa wanasheria wa Serikali ambalo lilikosekana huko nyuma.
Amewakumbusha Mawakili wa Serikali kwamba kuwa Wakili wa Serikali ni heshima kubwa na heshima ya kuwa Wakili inaendana na wajibu hivyo wanapaswa kuitumikia Serikali ipasavyo, kutumia sheria kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza ndani ya Serikali.
Awali Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amewataka watendaji kuhakikisha wanawatumia vizuri wanasheria waliopo kwenye rejesta ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata ushauri kabla hajaingia kwenye mikataba au kabla ya kuvunja mikataba ili wazingatie kanuni na taratibu.
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi amesema chama kitakuwa ni jukwaa la Mawakili kujadili masuala mbalimbali ya kisheria yakiwepo ya kimafunzo yanayohusiana na utoaji wa huduma za kisheria na kutatua malalamiko ya kisheria kutoka kwa wadu mbalimbali.
Naye Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Msalama Mkama ameishukuru Serikali kwa kuwa na maono ya mbali na kuanzisha Chama cha Mawakili wa Serikali ambacho kitakuwa kama jukwaa kwa Mawakili hao kujadili masuala yao ya msingi kwenye Sekta ya Sheria.
Bw. Mkama amesema kuwa chama hicho kitaiwezesha Serikali kuwaunganisha Mawakili na kujadili changamoto zao kwa pamoja na kuiwezesha Serikali kufahamu idadi na utendaji kazi wa Mawakili katika Wizara, Taasisi, Sekretariati za Mikoa na Halmashauri zote nchini.
“Chama kitawawezesha Mawakili kushirikishana katika ujuzi walio nao na kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi katika kusimamia mashauri ya Serikali kutoka kwenye taasisi zao na pia kutatua changamoto walizonazo kwa kutumia uzoefu walio nao.
Mkutano huo umehudhuriwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende, Mkurugenzi wa Mashtaka, Slyvester Mwakitalu, Viongozi waandamizi wastaafu wa Sekta ya Sheria nchini akiwemo Mtemi Andrew Chenge.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali