Hatumzuii Mtu kuanzisha Televisheni ya Mtandaoni-Msigwa
Na Grace Semfuko, MAELEZO
Septemba 28, 2022
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO Bw. Gerson Msigwa amesema Tanzania ni moja kati ya Nchi Duniani zenye vyombo vingi vya Habari na kwamba bado inaendelea kusajili vyombo hivyo ili viweze kuuhabarisha umma.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha watanzania wanapata habari kupitia vyombo hivyo huku Waandishi nao, wanakuwa huru katika kukusanya, kuchakata na kusambaza habari za ukweli ambapo Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya mwaka 2016 imeanisha masuala hayo.
Ameyasema hayo leo Septemba 28, 2022 Jijini Dar es Salaam aliposhiriki kwenye mahojiano katika kipindi cha Baragumu kinachorushwa na Televisheni ya Channel Ten ikiwa ni siku ya kimataifa ya upatikanaji wa habari kwa wote ambapo ameongeza kuwa, wingi huo wa vyombo vya habari umewekwa kwa makusudi ili watanzania wawe huru kupata habari huku waandishi nao waweze kufanya kazi zao kwa uhuru.
“Sisi Tanzania tumerahisisha sana, na nchi yetu ni moja kati ya nchi Duniani ambayo ina idadi kubwa ya vyombo vya habari, na tumefanya hivi makusudi ili watanzania wawe huru kupata habari, na Vyombo vya habari pia pamoja na waandishi wawe huru kufanya kazi zao, hivi ninavyozungumza nchi yetu ina idadi ya magazeti na majarida yaliyosajiliwa 303, TV za Mtandaoni zaidi ya 667 Redio za mtandaoni 23, redio za kawaida zaidi ya 210, na tunaruhusu hata leo ukitaka kuanzisha redio, unaanzisha, sasa zipo nchi ambazo zina vyombo vya habari havizidi hata vitano” amesema Bw. Msigwa.
Amesema jukumu la Serikali ni kufungua milango ya kuanzisha vyombo vya habari ambapo mtu yeyote anaruhusiwa kuanzisha ili mradi tu afuate sheria.
“Kuna sheria kwa mfano ya huduma za habari namba 12 ya mwaka 2016 tumeiweka pale kwa ajili ya kusimamia sekta ya habari lakini wakati huo huo tunawasikiliza wadau, mfano hivi karibuni Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo, Mheshimiwa Waziri Nape alishatoa maelekezo anasimamia utekelezaji” amesema Bw. Msigwa.
Mwisho.