Home » » TANZANIA, VENEZUELA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

TANZANIA, VENEZUELA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

Written By CCMdijitali on Monday, September 5, 2022 | September 05, 2022

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Venezuella zimesaini Hati za Makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kisiasa na mkataba wa ushirikiano katika nyanja mbalimbali baina ya nchi hizo. 

Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

“Tumesaini mikataba miwili ambapo mmoja unalenga kuendeleza majadiliano ya kisiasa (political consultation) lakini pia makubaliano ya kuwa na ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kichumi, nishati, afya, elimu na kilimo,” amesema Balozi Mulamula.

Kusainiwa kwa mikataba hiyo ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano kati ya Tanzania na Venezuela katika sekta za nishati, afya, elimu na kilimo kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo miwili ni hatua muhimu ya kudumisha na kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali baina ya Venezuela na Tanzania.

Mhe. Moura amewasili nchini leo akitokea Venezuela na atakuwepo nchini kwa siku mbili kwa ziara ya kikazi. 

Katika tukio jingine, Balozi Mulamula amekutana na kupokea barua za utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Kenya mwenye makazi yake Arusha, Bw. Dennis Mburu katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.


Baada ya kupokea barua za utambulisho kutoka kwa Bw. Mburu Balozi Mulamula amemuahidi ushirikiano kutoka Serikalini wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala ya biashara na uwekezaji pamoja na utalii.  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.



Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika (kushoto), Balozi Swahiba Mndeme pamoja na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Balozi Mindi Kasiga (kulia) wote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kikao cha Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Moura katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura kwa pamoja wakisaini Hati za Makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kisiasa na mkataba wa ushirikiano katika nyanja mbalimbali baina ya nchi hizo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Utiaji saini Hati hizo umeshuhudiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wengine ni  Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Swahiba Mndeme, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga wote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Konseli Mkuu wa Kenya mwenye makazi yake Arusha, Bw. Dennis Mburu. wengine pichani niMkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga na Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Ubalozi wa Kenya nchini katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Konseli Mkuu wa Kenya mwenye makazi yake Arusha, Bw. Dennis Mburu. wengine pichani niMkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga na Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Ubalozi wa Kenya nchini katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link