BILIONI 3.8 KUJENGA MADARASA 191 RUKWA- RC SENDIGA
Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amesema atahakikisha fedha zote zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya 191 kwenye shule za sekondari mkoani humo zinatumika kama ilivyokusudiwa ili wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023 waweze kuanza masomo yao kwa wakati.
Serikali ya Awamu ya Sita imeupatia mkoa wa Rukwa shilingi Bilioni Tatu na Milioni Mia Nane na Elfu Ishirini (3,820,000,000/-) kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa katika halmashauri nne za mkoa wa Rukwa ambapo kila darasa litajengwa kwa shilingi Milioni Ishirini kupitia mfumo wa “Force Account”.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (03 Oktoba,2023) ofisini kwake mjini Sumbawanga Mhe. Sendiga alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanapata mahala bora na salama kusomea.
“Natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kufuatilia kwa ukaribu ujenzi wa madarasa hayo ili yaweze kukamilika kwa muda yaani ndani ya siku Sabini na Tano (75) kama alivyoelekeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI na kwa ubora ulioelekezwa pamoja na kukamilisha utengenezaji wa madawati yake” alisisitiza Sendiga.
Katika taarifa yake, Mhe. Sendiga alisema mkoa umefanya maoteo ya Wanafunzi 26,655 wa kujiunga Kidato cha kwanza mwezi Januari, 2023. Maoteo hayo ni kutoka jumla ya watahiniwa 33,319 waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya msingi mwaka 2022 sawa na asilimia 80 ya ufaulu ambapo wanafunzi hao watahitaji jumla ya madarasa 534 ambapo madarasa yaliyopo ni 343 na upungufu ni madarasa 191.
Sendiga alitaja mchanganuo wa idadi ya vyumba 191 vya madarasa kwa kila Halmashauri kwenye mabano, Manispaa ya Sumbawanga (56) sawa na shilingi 1,120,000,000/= ,Halmashauri ya Nkasi (26) sawa na shilingi 520,000,000/= Halmashauri ya Sumbawanga (46) sawa na shilingi 920,000,000/= na Halmashauri ya Kalambo (63) sawa na shilingi 1,260,000,000/=.
Mwisho.