Baba Mtakatifu Papa Francis amtunuku Padre Richard Mjigwa, C.PP.S., kutoka Tanzania Nishani ya Msalaba wa Kanisa na Papa kutokana na huduma ya mawasiliano ya Kanisa kupitia Radio Vatican Idhaa ya Kiswahili.
Padre Mjigwa pia anahudumu katika Baraza la Kipapa la Mawasiliano kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican ni mtanzania wa pili kutunukiwa Nishani hiyo baada ya miaka 6 tangu Mtanzania wa kwanza aliyehudumu katika Baraza hilo, Mama Thabita Janeth Mhella kutunukiwa Nishani hiyo mwezi Septemba 2016.
Padre Mjigwa ambaye ni Mwanashirika wa Shirika la Damu Azizi, alikabidhiwa Nishani hiyo na Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano la Kipapa, Dkt. Andrea Tornielli kwa niaba ya Papa Francis kufuatia juhudi zake za kuhudumia jamii katika kueneza sauti na miongozo ya Papa katika lugha ya Kiswahili kupitia Radio Vatican kwenye mataifa yanayozungumza lugha hiyo.
Padre Mjigwa aliyezaliwa Tanzania mwaka 1964 alianza shughuli ya huduma ya uandishi wa habari kama mshirika mnamo mwaka 1994 hadi 1999 na baadaye kuanza rasmi katika Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kuanzia mwaka 2008 hadi sasa.
Katika hatua nyingine, Padre Mjigwa kwa niaba ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican alipokea Nishani ya maadhimisho ya miaka 30 ya Idhaa hiyo ambayo ilianzishwa rasmi Tarehe 27 Septemba 1992. Tuzo hiyo ameipokea wakati muafaka ambapo Lugha ya Kiswahili imeendelea kutambulika duniani kama lugha kuu mojawapo ya mawasiliano.
Utangazaji katika lugha ya Kiswahili kwenye Radio Vatican ulianza mapema mwezi Novemba 1961 baada ya Wamisionari wa Afrika (White Fathers) kuanza kuandaa makala kwa lugha ya Kiswahili kufuatia uzinduzi uliofanywa na Papa Mtakatifu Yohane XXIII na kupelekea kurushwa matangazo hayo ya kila siku kwa Afrika.
|
Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano la Kipapa, Dkt. Andrea Tornielli akimkabidhi Nishani ya Msalaba wa Kanisa na Papa, Padre Richard Mjigwa, (C.PP.S.) kutoka Tanzania kutokana na huduma ya mawasiliano ya Kanisa kupitia Radio Vatican Idhaa ya Kiswahili
|
| Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano la Kipapa, Dkt. Andrea Tornielli akimpongeza Padre Richard Mjigwa, (C.PP.S.) kutoka Tanzania baada ya kupokea Nishani ya Msalaba wa Kanisa na Papa, kutokana na huduma ya mawasiliano ya Kanisa kupitia Radio Vatican Idhaa ya Kiswahili
|
| Picha ya pamoja
|
|