Timu Zapambana Kufika Hatua 16 Bora SHIMIWI Tanga
Na Mwandishi Wetu, Tanga
RATIBA ya michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea kwa hatua ya makundi huku timu zikipambana kupapata nafasi katika hatua 16 bora.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya SHIMIWI, Apolo Kayungi amesema kutokana na ushiriki wa timu nyingi mwaka huu kumesababisha ratiba ipangwe kwa timu kucheza mfululizo ili kukamilisha hatua ya makundi kwa wakati, ambapo zinatakiwa kumalizika tarehe 7 Oktoba, 2022.
“Ratiba ni ngumu lakini ni kutokana na uwingi wa timu na muda wa mashindano kwani kama mlivyoona timu nyingi zimetoka mbali ikabidi ttuanze tarehe 2 Oktoba badala ya tarehe 1, na tukumbuke tarehe 5 Oktoba ni uzinduzi rasmi, ambapo pia kutakuwa na michezo michache hivyo kunasababisha kupungua pia kwa muda,” amesema Kayingi.
Hatahivyo, amesema baada ya kumalizika kwa hatua ya makundi itaingia hatua ya timu 16 bora ambao watapatikana kwa kila kundi kutoa timu mbili za juu, ambapo yapo makundi nane, na baadae tarehe 8 Oktoba zitafanyika mbio za riadha za mita mbalimbali.
Mchezaji Marko Mochuwa wa Idara ya Mahakama amesema mashindano haya yanaendeshwa vizuri, ambapo wachezaji wanafurahi kwani michezo hii inasababisha miili kuchangamka.
“Muda mwingi tunakuwa makazini na hii michezo sasa inasaidia kuchangamsha miili na akili zetu, kwa ajili hiyo mashindano ni mazuri mno kwa afya zetu,”amesema Marko.