Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Samoei Ruto amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya Siku mbili. Mhe. Dkt. Ruto ambaye ameambatana na mke wake Mama Rachel Ruto, amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wa jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam Mhe. Dkt. Ruto alikagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake na kuelekea hotelini kwa mapumziko.
Tarehe 10 Oktoba 2022 asubuhi, Mhe. Dkt. Ruto atawasili katika Ikulu ya Dar es salam ambapo atpokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao watakuwa na mazungumzo rasmi ambayo yatakayohusisha wajumbe wa pande zote mbili.
Baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo rasmi viongozi hao watazungumza na waandishi wa habari kuhusiana na walichojadili katika ziara hiyo na baadaye watahudhuria dhifa ya kitaifa ambayo Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuandalia mgeni wake Mhe. Dkt. Ruto.
baada ya kumalizika kwa Dhifa hiyo ya Kitaifa, Mhe. Dkt. Ruto na ujumbe wake wanatarajiwa kuondoka kurejea nchini Kenya.