Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kunufaika kiuchumi kupitia sekta hiyo.
Waziri Dkt. Tax amesema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya ASSECO ya Poland Bw. Adam Goral, inayojishughulisha na masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yenye nia ya kuwekeza nchini.
Akizungumza na Rais huyo, Mhe. Dkt. Tax amemweleza nia ya Serikali ya Tanzania ya kutaka kujiimarisha kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupitia teknolojia hiyo nchi iweze kunufaika kiuchumi.
Mhe. Waziri amesema kuwa, katika ulimwengu wa sasa mifumo mingi ya utendaji imebadilika ambapo kazi nyingi hukamilishwa kwa kutumia vifaa vya kisasa kama simu, kompyuta na mtandao. Hivyo unahitajika uwekezaji wenye tija hususan kwenye eneo la usalama wa taarifa za watumiaji.
Ameongeza kuwa matumizi ya tehama nchini yameendelea kukua siku hadi siku ambapo taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali, za Fedha, Shule, Hospitali na nyingine hutegemea teknolojia ya uhakika na salama ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija.
Amesema mbali na mchango mkubwa wa tehama katika ukuaji wa uchumi nchini pia imeendelea kuchangia uzalishaji wa ajira kwa watanzania hususan vijana.
"Tanzania inayo nia ya dhati ya kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza na kunufaika kiuchumi kupitia matumizi ya tehama. Hata hivyo jambo muhimu katika teknolojia hii ni usalama wa taarifa katika matumizi ya teknolojia hiyo. Hivyo, tungependa wawekezaji kulipa kipaumbele suala hili pale wanapokuja kuwekeza”, alisema Dkt. Tax.
Aidha, Mhe. Dkt tax ameahidi kuiunganisha taasisi hiyo na mamlaka husika nchini, ikiwemo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhusu nia yao ya kutaka kuwekeza nchini ili mazungumzo yaanze.
Kwa upande wake Rais wa Kampuni hiyo Bw. Goral amemshukuru Mhe. Waziri kwa kutembelea Kampuni hiyo na kusema kampuni yake inatengeneza software zake yenyewe na kuongoza kwa teknolojia kwa upande wa Ulaya mashariki ina nia ya dhati ya kuwekeza nchini na ipo tayari kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo mbalimbali ya tehama.
“Kampuni yetu ina nia ya dhati ya kuwekeza Tanzania na usalama wa matumizi ya mtandao ni kipaumbele chetu. Tayari tunayoo Program maalum ilianza mwaka 2020 inayoshughulikia usalama wa mitandao. Tupo tayari kubadilishana uzoefu na ujuzi na Tanzania” alisema Bw. Goral
Awali akitoa mada kwenye mkutano huo kuhusu hali ya matumizi ya teknolojia ya habari nchini, Mtaalam wa Tehama kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy amesema Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya tehama ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hadi sasa watanzania wanaomiliki simu ni milioni 28 na muamala ya simu imeingiza mapato ya zaidi Shilingi Trilion 20 kwa mwaka 2021 pekee.
Kampuni ya Asseco iliyoanzishwa mwaka 1991 hutoa mafunzo na ushauri kuhusu masuala ya tehama na kutengeneza software zake yenyewe. Tayari imewekeza katika Mabara sita na nchi 60 ulimwenguni zikiwemo Ethiopia, Nigeria, Togo na Botswana kwa upande wa Bara la Afrika.
Mhe. Dkt. Tax alikuwa nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine alitumia ziara hiyo kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji nchini.
Mkutano ukiendelea |
Rais wa Kampuni ya ASSECO, Dkt. Goral akizungumza wakati wa mkutano na Mhe. Dkt. Tax |
Wajumbe wengine wa Tanzania |
Ujumbe wa Serikali ya Poland akiwemo Balozi wa Poland nchini Tanzania (kushoto) |
Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy akiwasilisha mada kuhusu matumizi na changamoto za mtandao |
Wajumbe kutoka Tanzania wakati wa mkutano huo |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiagana na Rais wa Kampuni ya ASSECO, Dkt. Goral |