Home » » Watumishi fanyeni mazoezi ili kuimarisha Afya

Watumishi fanyeni mazoezi ili kuimarisha Afya

Written By CCMdijitali on Sunday, October 16, 2022 | October 16, 2022

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba amesema katika kuendeleza michezo nchini, kila Wizara, Idara, Wakala na taasisi za Serikali zinapaswa kuwa na mipango endelevu ya michezo mahali pa kazi ili watumishi waweze kufanya mazoezi kwa ajili ya kujenga afya ya mwili na akili.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kufanya mazoezi ya kila Jumamosi moja kwa mwezi hatua inayowasaidia watumishi kujenga tabia ya kufanya mazoezi kila wanapopata nafasi ili kuimarisha afya zao.

Mhe. Mgumba ametoa kauli hiyo Oktoba 15, 2022 wakati anaahirisha mashindano ya 36 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamefanyika kuanzia Oktoba 1, 2022 jijini Tanga.

“Ndugu wanamichezo, nawasihi na kuwasisitiza muendelee na jitihada za kuhakikisha michezo inasimamiwa ipasavyo na kudumishwa mahali pa kazi, niungane na wageni rasmi waliowahi kupata heshima hii ya kufunga michezo ya SHIMIWI ambayo ni ya watumishi wa Umma inazidi kuboresha afya zetu za mwili na akili” amesema Mhe. Mgumba.

Mhe. Mgumba amesema kuwa faida za kuwaruhusu watumishi hao wa umma kuja kushiriki mashindano hayo mkoani Tanga na kuongeza kuwa faida za kuwaruhusu viongozi wataziona watumishi hao watakaporudi kazini ambapo matumaini yake watakuwa wachangamfu, wenye afya njema na ari kubwa ya kufanya kazi.

Aidha, Mhe. Mgumba ameupongeza uongozi wa SHIMIWI na kuwasihi waendeleze mpango wa kuwa na eneo maalum la michezo mkoani Dodoma kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango mwaka 2021 wakati anafungua mashindano ya 35 ya SHIMIWI mkoani Morogoro.

Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa mipango iliyobuniwa ikamilishwe kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kituo kitakapojengwa kiwe ni maalumu kwa ajili ya watumishi wa umma na kwa faida ya vizazi vijavyo na kuwashirikisha watumishi wa Tanzania Zanzibar katika mashindano ya SHIMIWI kuanzia mwakani 2023 ili kuendelea kudumisha Muungano.

Naye Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Bw. Daniel Mwalusamba ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa kwa ushirikiano wao wakati wote wa maandalizi ya michezo hiyo hadi kufikia kilele pamoja na viongozi wote sehemu za kazi kwa kuwaruhusu watumishi wanamichezo kushiriki kwa ufanisi mkubwa kwa ajili ya kujenga afya zao.

Vilevile amewaomba viongozi wote sehemu za kazi waendelee kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha watumishi wa umma kushiriki kwenye michezo na mazoezi ili waweze kujenga afya zao na hatimaye kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bi. Emma Lyimo ambaye pia alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa mashindano hayo ni utekelezaji wa Sera ya Michezo nchini.

Aidha, Bi. Emma ametoa wito kwa Shirikisho la SHIMIWI kuendelea kuzingatia taratibu za mashindano hayo na yaendeshwe kwa haki pamoja na kushirikiana na Baraza la Michezo katika kuendesha mashindano hayo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za shirikisho pamoja na sharia za nchi ili kuleta amani na haki miongoni mwa wafanyakazi.

Mashindano ya SHIMIWI 2022 yamefanyika kwa siku 15 kuanzia Oktoba 1-15, 2022 yameshirikisha wanamichezo 2510 kutoka klabu 67 ambazo ni timu za Wizara, Wakala, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa.

MWISHO


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba akifunga mashindano ya 36 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamefanyika kuanzia Oktoba 1-15, 2022 jijini Tanga.



Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) Taifa Bw. Daniel Mwalusamba akitoa katika hafla ya kufunga mashindano ya 36 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamefanyika kuanzia Oktoba 1-15, 2022 jijini Tanga.



Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bi. Emma Lyimo ambaye pia alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi wakati wa hafla ya kufunga mashindano ya 36 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamefanyika kuanzia Oktoba 1-15, 2022 jijini Tanga.



Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link