Home » » WAZIRI MKUU NA MAKAMU WA PILI WA RAIS- SENSA

WAZIRI MKUU NA MAKAMU WA PILI WA RAIS- SENSA

Written By CCMdijitali on Tuesday, October 11, 2022 | October 11, 2022

 

Kukamilika kwa zoezi la Sensa ya watu na Makazi limechangiwa kwa kiasi kikubwa na miongozo iliyokuwa ikitolewa na viongozi Wakuu wa nchi.

Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa kamati kuu ya Taifa ya Sensa ya watu na Makaazi, Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa katika kikao kazi kilichofanyika Ukumbi wa Hoteli Verde, Mtoni jijini Zanzibar.

Alisema, kamati imeridhishwa na taarifa za matokeo ya awali ya sensa ya watu na Makaazi ambayo imeoneshwa asalimia 98% ya watanzania wamehesabiwa mijini na vijini.

Mhe. Majaaliwa alisema Watanzania wengi waliona umuhimu wa kuhesabiwa na kutoa ushirikiano mkubwa kwa makarani, hali hii itairahisishia Serikali kufikia malengo iliyojiwekea kwa wananchi wake.

Aidha, alisema asilimia mbili 2% iliyobakia ni ya wale ambao hawakuhesabiwa kutokana na mazingira ya kutatanisha waliyokua nayo. Hata hivyo, watu hao bado wanakwenda katika Ofisi za Serikali za Mitaa waliopo kwa lengo la kutaka kuhesabiwa ingawa muda wake umeisha.

Akizungumzia kuhusu kutolewa kwa taarifa Rasmi ya Sensa ya watu na Makaazi, Mhe Majaaliwa alisema kwamba taarifa hiyo inatarajiwa kutolewa na Rais wa Jamuhiri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ifikapo tarehe 31 mwezi huu katika Uwanja wa Jamuhuri, Mkoani Dodoma.

Alisema katika hafla hiyo, makundi mbali mbali yanatarajiwa kualikwa wakiwemo viongozi wastaafu, viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama Vya Siasa, Mashirika binafsi na wageni kutoka nchi mbali mbali pamoja na wananchi kwa ujumla.

Alisema, zoezi la uwekaji wa anuani za Makaazi katika miji na vijiji litakuwa endelevu hivyo amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na viongozi wa vijiji kuendelea kulisimamia zoezi hili katika sehemu zote zinazoendelea kujengwa.

Nae Mwenyekiti mwenza wa kamati hio ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza kuwa haikua kazi rahisi sana kukamilisha zoezi hilo, kwani imepitia katika changamato na nyakati tofauti lakini kupitia hekma na busara za viongozi pamoja na ushirikiano wa wananchi jambo hili limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Aidha, Mhe. Hemed aliwashukuru watanzania wote na Wadau mbali mbali walioshiriki katika jambo hili ambalo litairahisishia Serikali kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Hata hivyo, aliwataka viongozi kuendelea kujitolea katika utendaji kazi kwa kulipambania Taifa pamoja na kuwataka kila mmoja kujifunza kupitia jambo hili kwani litabakia kuwa ni historia kwa vizazi vya Sasa na baadae.

……………………..

Ali Moh’d

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

11.10.2022




 

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link