Na Shamimu Nyaki
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakubu amefungua kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo leo Agosti 27, 2023 mkoani Njombe ambapo ametoa maagizo manne makubwa kwa maafisa hao ikiwemo kuongeza ushiriki wa jamii katika michezo na kuibua vipaji vya Utamaduni, Sanaa na michezo katika maeneo yao.
Amewaagiza maafisa hao, kuandaa mikakati itakayosaidia vijana kutumia majukwaa mbalimbali kuonesha vipaji vyao pamoja na kuandaa mkakati wa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili ambao umeanza kujitokeza katika jamii.
"Serikali inaendelea kuongeza wataalamu wa michezo kupitia Chuo Cha Michezo Malya ambacho sasa kinafanyiwa maboresho makubwa ikiwemo ujenzi wa hosteli mpya ambayo itasaidia ongezeko la udahili wa wanafunzi chuoni hapo", amesema Katibu Mkuu Yakubu.
Bw. Yakubu ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha Kitengo cha Utamaduni na Michezo kinatengewa bajeti ya kutosha ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Katibu Mkuu Yakubu ametumia nafasi hiyo kugawa vifaa vya michezo ikiwemo mipira 54 ya mchezo wa Mpira wa Miguu, Kikapu na Wavu ambayo itagawiwa kwa mikoa yote nchini kwa ajili ya mashindano ya Samia Cup yanayotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.