Watumishi wa Wizara ya Fedha wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuzingatia sheria, kanuni, taratibu pamoja na miongozo katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya wizara ili kuleta tija katika Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande, wakati akifungua kikao kazi cha Watumishi wa Wizara hiyo kwa niaba ya Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini - IRDP, jijini Dodoma.
Alisema kuwa ni lazima kila mtumishi kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali pamoja na Wizara ikiwa ni kuziishi tunu za Wizara ikiwemo uadilifu katika utekelezaji wa majukumu.
‘‘Tutambue kuwa Wizara ya Fedha ni moyo wa nchi yetu. Wizara ya Fedha ikiyumba, nchi inayumba. Hivyo, ni muhimu kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, weledi, ubunifu, uwazi na kuwajibika pale tunapoenda kinyume na misingi ya utawalabora na utawala wa sheria, ili kuleta tija katika taasisi yetu na Taifa letu kwa ujumla’’, alisema Mhe. Chande.
Aidha alisisitiza umuhimu wa mawasiliano katika utekelezaji wa majukumu ikiwa ni pamoja na utoaji, upokeaji, usambazaji na utunzaji wa taarifa zinazohusu majukumu ya Wizara uzingatie misingi ya usiri pamoja mifumo na njia sahihi za mawasiliano.
‘‘Uthabiti katika mawasiliano ni muhimu kwa kila mmoja wetu ili kudumisha misingi ya uelewa na uwajibikaji wa pamoja. Teknolojia imerahisisha sana mifumo na njia za mawasiliano. Hata hivyo, kihatarishi kikubwa ni ukosefu wa uadilifu katika matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kutoa, kupokea, kusambaza na kutunza taarifa za kiofisi ili kulinda heshima ya Wizara yetu na Taifa kwa ujumla,’’alisisitiza Mhe. Chande.
Aidha alisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mali za Serikali kwa kusimamia sera, sheria, kanuni, miongozo na mifumo ya TEHAMA katika usimamizi wa mali za Serikali pamoja na kuongeza ubunifu na weledi katika eneo la usimamizi wa fedha za umma kwa kujenga uwezo na kuziba mianya ya opotevu wa mapato na matumizi mabaya ya fedha za umma.
‘‘Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa wabunifu zaidi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu. Mafunzo yanayolenga kuongeza ujuzi katika maeneo ya usimamizi wa fedha za umma yapewe kipaumbele ili kuchochea ubunifu mahali pa kazi,’’ alisema Mhe. Nchemba.
Alihitimisha kwa kuwapongeza watumishi kwa ushiriki makini katika maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024 na kutoa rai kwa kila mmoja kusimamia eneo lake ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba amepongeza watumishi wote wa Wizara makao makuu na ofisi za mikoa kwa kuhitimisha vyema utekelezaji wa mpango na bajeti ya 2022/23.
‘’Pamoja na athari za UVIKO 19 na mgogoro kati ya Urusi na Ukraine kuendelea kuathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii hapa nchini, tumefanikiwa kufikia shabaha za bajeti ya serikali kwa asilimia 98.7. Mafanikio haya yametokana na juhudi zenu pamoja na watumishi wa Mamlaka nyingine za serikali’’, alisema Dk. Mwamba.
Alisema mwaka 2022/2023, Wizara ilitekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya msingi ya usimamizi wa masuala ya mipango, uchumi na fedha kutokana na mshikamano na ushirikiano uliopo miongoni mwa watumishi na viongozi wa Wizara.
‘‘Maeneo tuliyofanya vizuri zaidi ni kuhudumia deni la serikali kwa wakati, kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kwa sasa na kulipa mishahara ya watumishi kwa wakati hivyo nitoe wito kwa watumishi wenzangu kuimarisha upendo, uwazi, ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja ili kujenga taasisi imara, endelevu na bunifu.’’ alisema Dkt. Mwamba.
Alisema kuwa uongozi wa Wizara unaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza ari, bidii na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Alifafanua kuwa katika mwaka 2022/2023, Wizara imefanikisha kupandisha madaraja watumishi 162 na kubadilisha kada watumishi 6, kugharamia mafunzo ya muda mrefu watumishi 60 na mafunzo ya muda mfupi watumishi 285 pamoja na kuendelea kuboresha mazingara ya TEHAMA kwa kuanza kutumia mifumo mbalimbali inayorahisisha upatikana wa huduma na taarifa na kupunguza matumizi ya karatasi.
Kwa upande wao Manaibu Katibu Mkuu Bi. Jenifa Omolo na Elijah Mwandumbya walisisitiza watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na kuwa na nidhamu ya kazi pamoja na ubunifu ili kuhakikisha kuwa changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa namna bora.
Pia waliwapongeza watumishi wa Wizara hiyo kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuahidi kuwa uongozi wa Wizara hiyo utaendelea kushirikiana nao ili kuwa na mazingira ya kazi rafiki kwa kila mtumishi kuweza kutimiza wajibu wake.
Wizara ya Fedha imekutana na watumishi hao ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kukutana mwanzoni mwa mwaka wa fedha kutafakari kwa pamoja yaliyojiri katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Serikali kwa mwaka uliotangulia na kushirikishana mikakati ya utekelezaji wa vipaumbele kwa mwaka wa fedha uliopo.