Home » » SERIKALI IMETENGA BILIONI 1.5 KUIMARISHA HUDUMA YA UZAZI SALAMA ZANZIBAR.

SERIKALI IMETENGA BILIONI 1.5 KUIMARISHA HUDUMA YA UZAZI SALAMA ZANZIBAR.

Written By CCMdijitali on Saturday, August 26, 2023 | August 26, 2023

Zanzibar,

26 Agosti, 2023

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesifu jitihada za wadau wa maendeleo wakiwemo Mashirika ya Kimataifa, taasisi binafsi, makampuni na wahisani mbalimbali wanavyojitokeza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo, viwanja vya Maisra Suleiman alipozungumza kwenye kampeni ya “Uzazi ni Maisha” iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya Zanzibar na Shirika la Kimataifa la Amref Afika, tawi la Tanzania yenye lengo la kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga Zanzibar.

“Kwa dhati kabisa napenda niwashukuru Amref Health Africa kwa kutoa msaada wa gari (Mobile van) ambayo itakuwa msaada muhimu kwa Wizara ya Afya kwenye shughuli mbalimbali zikiwemo kusafirisha wataalamu, kusafirisha sampuli na kutoa huduma za upimaji na ushauri nasaha kwa wananchi katika vituo tofauti vya afya hapa Zanzibar” alieleza Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alisema, wadau hao wa maendeleo wamekua na mchango mkubwa kwa Serikali hasa kwenye masuala ya jamii na maendeleo kupitia sekta za Afya, Elimu na huduma za upatikanaji wa maji safi na Salama.

Aidha, alilipongeza Shirika la Amref kwa jitihada zao za kuanzisha kampeni za “Uzazi ni Maisha” zilizojumuisha matembezi ya mbio fupi na matembezi ya hiari, yaliyoanzia Kiembe Samaki kwa Butros Wilaya ya Magharibi B na kumalizikia viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Alisema, uamuzi huo ni jitihada za kuunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza na kuepusha vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga ambapo alieleza bado kiwango cha changamoto hiyo kipo juu.

Rais Dk. Mwinyi alieleza takwimu zinaonesha vifo vya kina mama 134 kati ya vizazi hai 100,000 kwa mwaka na vifo 28 vya watoto wachanga kati ya vizazi hai 1,000 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017, husababishwa na changamoto za huduma duni za mama na mtoto katika hospitali na vituo vya afya zikiwemo uhaba wa wahudumu na tatizo la kukosekana kwa dawa.

Dk. Mwinyi, alieleza matumaini yake kupitia kampeni hiyo, kwamba Serikali itaongeza vifaa tiba kwa vituo vya afya 28, sawa na asilimia 40.5 ya vituo vyote 69 vinavyotoa huduma za mama na mtoto Zanzibar. 

Pia, alieleza jitihada za Seriklali kuimarisha huduma za afya ya msingi kwa ajili ya uzazi salama, italeta mafanikio makubwa ya kulinda maisha ya mama na mtoto.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Zanzibar Hassan Hafidh alisema lengo la kuanzishwa kwa kampeni ya “Uzazi ni Maisha” ni kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto nchini.

Alisema, katika kulikabili tatizo hilo kivitendo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati madhubuti ikiwemo kuwachukulia hatua kali za kisheria na nidhamu watumishi wote wa sekta ya Afya wanaokiuka sheria na taratibu za utumishi wao kutokana na uzembe kazini, kauli chafu, utovu wa nidhamu unaosababisha athari mbaya kwa mama na watoto hasa wakati wa kujifungua. Aidha alieleza Wizara imefanikiwa kuzizibidhi hali hiyo kwa asilimi kubwa.

Naye, Mwakilishi mkaazi wa Shirika la Amref Afika kwa upande wa Tanzania, Dk. Folence Temu alisema lengo la kuanzishwa kampeni hiyo ya “Uzazi ni maisha ni kukusanya shilingi Bilioni moja kwajili ya kununuliwa vifaa tiba vya hospitali na vituo vya afya 69 vinavyotoa huduma za mama na mtoto, Zanzibar.

Alisema, wakiwa kwenye mwaka wa pili wa kampeni yao, Shirika la Amref tayari limefanikiwa kukusanya milioni 557 na wamepokea ahadi za shilingi milioni 883 ambayo itafikisha lengo la kampeni hiyo kufikia 2024.

Kampeni ya “Uzazi ni Maisha” ilianza mwaka jana na inatarajiwa kukamilika mwakani inatekelezwa kwa kaulimbiu isemayo ”Changia vifaa tiba kwa uzazi salama” ambayo imechangia kufikia malengo ya kuanzishwa kwake mwaka wa pili sasa wa utekelezaji wake. 


IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link