Kuwepo kwa mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya lazima Zanzibar (ZIQUE) pamoja na miradi mengine kumeleta mafanikio makubwa ikiwemo kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yaliyopelekea kuimarika kwa ufaulu kwa wanafunzi katika mitihani yao ya Taifa hasa katika masomo ya Sayansi.
Akizundua Mradi wa ZIQUE huko katika Viwanja vya Skuli ya Msingi ya Salim Turkey Mpendae, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Miradi hii imesaidia sana kufikisha na kuboresha huduma ya elimu katika maeneo mbali mbali nchini yakiwemo katika visiwa vidogo vidogo Unguja na Pemba ambapo kasi ya ufaulu kwa mitihani ya kidato cha nne imeongezeka na kufikia asilimia 72.2 kwa mwaka 2022.
Ameeleza kuwa uwepo wa vituo vya ubunifu wa kisayansi na kutolewa mafunzo kwa walimu hasa wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kingereza kumechangia sana kuimarika kwa ubora wa elimu inayotolewa nchini.
Aidha Mhe Hemed amefahamisha kuwa kutokana na kasi ya uimarishaji wa miundombinu ya Elimu matarajio ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa tatizo la uhaba wa nafasi kwa Wanafunzi kuingia Skuli Awamu mbili linakwenda kumalizika na kutoa nafasi kwa wanafuzi wa Zanzibar kusoma kwa Awamu mmoja tu.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa Mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya lazima Zanzibar umelenga pia kuwajengea uwezo zaidi walimu ili kuimarisha ufanisi wa kazi zao katika kusomesha kwa kufuata mitaala ya umahiri (CBC) na kuwasihi walimu kushiriki ili kwenda sambamba na mitaala inayozingatia umahiri na kupelekea wanafunzi kufanya vizuri zaidi kwa maendeleo yao, jamii na Taifa kwa ujumla.
Sambamba na hayo ameutaka uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kusimamia vyema utekelezaji wa Mradi huo na miradi Mengine sambamba na kuwataka wananchi kuendelea kuitunza miundombinu inayojengwa na Serikali ili iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa mradi wa ZIQUE utatekelezwa kwa makubaliano waliyokubaliana na Benki ya Dunia na utakamilika ndani ya miaka mitatu badala ya miaka sita ya makubaliano ya awali.
Waziri Lela amefahamisha kuwa Wizara ya Elimu imejipanga kumyanyua mtoto wa kike hasa katika masomo ya Sayansi na kuongeza ubora na kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Akitoa maelezo ya mradi huo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Ndg. Khamis Abdulla Said amesema mradi wa ZIQUE utaboresha elimu ya lazima na mfumo wa elimu kwa kuzalisha wanafunzi wenye ujuzi, maarifa, mafunzo ya walimu kazini, matumizi ya Teknolojia na kupitia mitaala ya Vyuo vya Ualimu ili mitaala hiyo iendane na ufundishaji wa kidijitali.
Amesema kuwa Wizara ya Elimu imejipanga kuvifanyia ukarabati Vyuo viwili vya Ualimu kwa Unguja na Pemba sambamba na kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa Takwimu na matumizi yake pamoja na uwajibikaji kwa Watendaji wa Wizara ya elimu.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa amesema mradi wa kuimarisha ubora wa Elimu ya lazima Zanzibar utaondoa changmoto ya katika sekta ya elimu na kuhakikisha Wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia Tanzania Bw. Nathan Balete kwa kuzingatia umuhimu wa Elimu ndiko kulikoifanya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzindua mradi wa ZIQUE ili kusaidia uboreshaji wa miundombinu elimu ya lazima, kukuza mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kuimarisha matumizi ya Teknolojia Maskulini.
Amesema Benki ya Dunia ipo tayari kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha mradi wa ZIQUE na miradi mengine inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kutoa matunda chanya yaliyokusudiwa.
……………………
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
26 Septemba,2023