WAZIRI SILAA AIPONGEZA NHC UTEKELEZAJI MIRADI
Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa utekelezaji mzuri wa miradi yake katika maeneo mbalimbali.
"Shirika limejipanga vizuri na kazi imefanyika vizuri na pongezi ni nyingi kuliko kukosoa". alisema Silaa.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi ya 7 11 Kawe, Samia Housing Scheme Phase I pamoja na mradi wa Morocco Square tarehe 11 Sept 2023 Waziri Silaa amesema, pamoja na NHC kutekeleza miradi mikubwa jijini Dar es salaam lakini shrika hilo linatakiwa kupeleka mradi wa Samia aliouelezea kuwa una sura ya kitaifa kwenye majiji makubwa yenye uhitaji wa nyumba
"Nataka mradi wa Samia uende kwenye mikoa mingine yenye uhitaji na kuwa na mradi wenye jina la Samia lazima uwe na sura ya kitaifa kuwe na kuwe na plan kubwa ya maeneo mengi" alisema.
Akielezea mradi wa Morocco Square, pamoja na kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo ameeleza kuwa, umefikia wakati sasa kwa shirika la NHC kuongeza uwekezaji wa miradi ya nyumba ili watanzania wapate nyumba za kupanga na kununua.
" Tuna nyumba nyingi katika prime area ni nyumba za chini anakaa mpangaji mmoja ni wakati sasa kuongeza uwekezaji katika miradi ya nyumba ili ifike wakati nyunba ziwe nyingi na watanzania wengi wapate nyumba za kununua na kupanga" alisema Wazri Silaa.
"Ninyi mnafahamu pressure ya nyumba za NHC ni kubwa na hizi re-development mhakikishe mnatengeneza mpango wa kuwa maeneo yote, tunataka kuona Upanga, City Centre ikiwa na nyumba, wale waliokiwa wanajenga miaka ile ya 70 na 60 zile nyumba za ghorofa 3 walikuwa wanajenga kwa popukation ya watu milioni 3 na sasa tuko milioni 61 tunatarajia re-development inafanyika kwenye maeneo mengi yenye uhitaji" alisema.
Akigeukia mradi wa 7 11 Kawe uliosimama kwa muda mrefu, Waziri Silaa amesema angependa kuona ndoto ya Rais Samia inatimia kwa kukamilika mradi huo.
"Kusimama kwa mradi ni changamoto na kikubwa ni kuhakikisha mazungunzo yanafika mwisho kwa kuwa kuendelea kuchelewa gharama inaongezeka. Nitahakikisha mazungumzo yanafika mwisho na mradi unaendelea oktoba 2023. Mradi uishe na ulete faida na tija kwa uchumi" alisema.
Aidha, Silaa aliguasia sera ya ubia ya NHC ambapo alisema shirika hilo linatakiwa kuangalia mpango huo na kueleza kuwa, haiwezekani kuendelea wenyewe ndani ya taifa kwa kutegemea mitaji ya ndani au mikopo ya benki.
‘’Wako watu wana mitaji na sera ya ubia inaenda sambamba sera ya ardhi inayofanyiwa marejeo ili kuwa na sura nzuri ya umiliki wa nyumba ili watu wenye mitaji yao nje na ndani nchi kuweza kuja kumiliki nyumba na kupanga’’. Alisema Silaa
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdalah alieleza kuwa, mradi wa Moroko square umeenda vizuri kutokana na maeneo ya jengo hilo kupangishwa ambapo alisema kati ya nyumba mia moja za mradi huo nyumba arobaini tayari zimepangishwa.
" Tunategemea baada ya kupata wapangaji mradi utaingiza milioni 850 kwa mwezi na huu ni katika miradi ya mfano ambapo zamani kulikuwa na nyumba tatu lakini sasa kuna eneo kubwa la shoping mall, hoteli na Tower mbili za ofisi na makazi mia moja lakini tungeacha tungekuwa na familia tatu tu". Alisema Hamad.
----------------------------MWISHO--------------------------------
Muonekano wa maendeleo ya ujenzi wa Samia Housing Scheme uliopo Kawe jijini Dar es Salaam (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI) |