BALOZI WA JAPAN NCHINI TANZANIA ATEMBELEA MKOANI NJOMBE NA KUTAMBULISHWA FURSA ZINAZOPATIKANA NDANI YA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akiteta jambo na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa |
Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka ofisini kwake leo Oktoba 26, 2023 na kujadili masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Moja ya sekta zilizoguswa kwenye mazungumzo ya viongozi hao wawili ni pamoja na kilimo, uwekezaji na utunzaji wa mazingira na uboresheji wa miundombinu ya zahanati za Mkoa wa Njombe.
Katika mazungumzo yao balozi huyo amesema serikali ya Japan imekuwa ikiendelea kuisaidia Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo Ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Itambo Wilayani Wanging'ombe,Ujenzi wa hostel na vyoo kwenye shule mbalimbali na wataendelea kusaidia katika nyanja nyingine.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe.Antony Mtaka pamoja na katibu tawala Mkoa Bi.Judica Omary wameshukuru Kwa jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya Japan katika kutekeleza miradi hiyo huku wakiomba kuendelea kwa mashirikiano katika fursa zilizopo mkoani Njombe.
Aidha, Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa amepata nafasi ya kutembelea mabanda mbalimbali ya wajasiliamari katika maonesho ya SIDO Kitaifa yanayoendelea mkoani Njombe.
Pia viongozi wa Mkoa wa Njombe akiwemo Katibu Tawala Bi. Judica Omari, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Kissa Gwakisa, Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda pamoja na Katibu Tawala Wilaya ya Njombe Bi. Agatha Mhahiki wameshiki mapokezi ya kiongozi huyo.